Habari za Kitaifa

Madiwani Kisii, Laikipia washikana mashati

February 21st, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

KIZAAZAA kilishuhudiwa katika mabunge ya kaunti za Kisii na Laikipia mnamo Jumatano madiwani wa kaunti hizo waliporushiana maneno na hata kutishia kulimana makonde.

Vimbwanga hivyo vilijiri kufuatia tofauti zilizozuka baina yao walipokuwa wakijadili hoja kuhusu kung’atuliwa kwa Naibu Gavana na Kiongozi wa Wachache Bungeni mtawalia.

Katika Kaunti ya Kisii, madiwani wanaopinga kung’atuliwa afisini kwa Naibu Gavana Dkt Robert Monda walianza kupinga uamuzi wa Spika Philip Nyanumba kuruhusu ukusanyaji wa maoni ya umma kuhusu mapendekezo hayo.

Awali, mswada huo uliodhaminiwa na diwani wa Ichuni Wycliffe Siocha ulikuwa umesomwa bungeni lakini Kiongozi wa Wengi Henry Moracha alimwomba spika Nyanumba aruhusu wananchi watoe maoni yao kuuhusu.

Ombi hilo lilipokubalika, madiwani wanaoegemea upande wa Dkt Monda walianza kumshtumu spika na kumtuhumu kwamba alikuwa akichukua maagizo kutoka kwa Bw Moracha.

Kufuatia ubishi wao, madiwani hao walianza kuondoka Bungeni kama ishara ya kuonyesha kutoridhishwa kwao. Mmoja wa madiwani aliwamwagia wenzao maji ya chupa na jambo hilo liliibua mvutano uliowafanya waanze kuitana majina yasiyoweza kuchapishika.

Vikao hivyo vilipoahirishwa, madiwani hao walifuatana hadi nje ya majengo ya Bunge wakinyosheana vidole huku wakialikana  kwenye vita.

Wakihutubia wanahabari baada ya sarakasi hizo, madiwani wanaomuunga mkono Dkt Monda walisema sababu zilizoibuliwa na wenzao za kutaka kumtimua afisini mbunge huyo wa zamani wa Nyaribari Chache hazikuwa na msingi wowote.

“Tumeshangazwa na sababu walizoleta za kumng’atua Dkt Monda. Nataka kuwahakikishia wakazi wa Kisii kuwa Mswada huu ni “mfu” jinsi ulivyowasilishwa. Dkt Monda yuko salama,” MCA wa Masimba Bouse Mairura alisema huku akiongeza kuwa Katiba haikufuatwa kwenye utengenezwaji wa mswada huo.

Katika Kaunti ya Laikipia, madiwani walianza kutofautiana wakilalamikia notisi ya kutaka kunng’atua wadhfani Kiongozi wa Wachache katika Bunge hilo Parleto Lokipien.

Notisi hiyo ilitolewa na Spika Lantano Naabala. Fujo hizo zilisababisha kulemazwa kwa shughuli katika bunge hilo kwa siku mbili mfululizo.

Ilibidi maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia (GSU) kuitwa ili kudhibiti hali.

“Yale ambayo yamefanyika yametushtua sisi. Kuwa tuna Bunge ambalo halifuati sheria. Hata kumwondoa Kiongozi wa Wachache, tunahitaji sheria. Hili ni Bunge la sheria na lenye utaratibu unaofaa kufuatwa. Ndio maana tunasema kukosewa haki mahali fulani ni kukosewa haki katika sehemu zote za ulimwengu,” akasema diwani wa Githiga Gitahi Macharia.