Habari za Kaunti

Madiwani Kisii wamkaidi Arati, waendelea na hoja ya kumng’atua Dkt Monda

February 29th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

MADIWANI (MCAs) wanaotaka kumng’atua mamlakani Naibu Gavana wa Kisii Robert Monda wamekaidi rai ya gavana Simba Arati ya kuwataka kutomjadili naibu wake huyo katika Bunge la Kaunti.

Mnamo Jumatano, gavana Arati aliwasihi MCAs hao wampe nafasi azike tofauti zake na Dkt Monda nje ya Bunge lakini madiwani hao wamekaa ngumu kwani Alhamisi asubuhi, waliendelea na mipango yao na wakajadili hoja hiyo.

Taifa Leo imebaini kuwa Bw Arati alikutana na MCAs hao nyumbani kwake mnamo Jumatano usiku kuwaomba waondoe hoja hiyo lakini wakamkaidi.

Madiwani hao hata walikataa kuwahutubia wanahabari walioitwa kwa gavana na walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine.

Gavana Arati alitoa rai hiyo kwa madiwani baada ya kukutana na maaskofu na wachungaji wa makanisa na madhehebu mbali mbali siku ya Jumatano.

Kwa sasa, mawakili wa Dkt Monda, wakiongozwa na wakili aliyemwakilisha Rais William Ruto katika kesi ya jinai kule ICC Katwa Kigen na mwenzake Wilkins Ochoki wanajibu shtuma zilizoibuliwa dhidi ya Dkt Monda.

Dkt Monda na mkewe Joyce Monda wamo bungeni na wanafuatilia mjadala kuhusu hoja hiyo kwa ukaribu.

Dkt Monda tayari amekana shtuma za ufisadi na matumizi mabaya ya afisi yake.

Mbunge huyo wa zamani wa Nyaribari Chache amefutilia mbali madai kuwa pesa alizopokea kwenye simu yake, zinazodaiwa kuwa ni hongo si kweli na zilikuwa za kulipa deni aliyokuwa amempa rafikiye.

Diwani wa Ichuni Wycliffe Siocha ndiye aliyeleta hoja ya kutaka “kumumwagia unga” Dkt Monda.

Cha kushangaza ni kuwa Bw Siocha anatoka ukoo mmoja na Dkt Monda (Abanyaribari) na hatua yake ya kutaka kiongozi kutoka ukoo wake “amwage unga” ilifasiriwa na wengi kama “usaliti”

Siasa za viti vya kaunti katika jamii ya Abagusii zimejengeka pakubwa katika kigezo cha ukoo na kila ukoo hujaribu kutetea mtu wao anapoandamwa kisiasa kinyume na alivyofanya Bw Siocha.

Kufuatia kwenda kinyume na mapenzi ya watu wa ukoo wake, Bw Siocha amekuwa akipokea kashfa za kila aina kutoka kwa watu wa Nyaribari kwa kuleta hoja hiyo.

Ili kutetea hoja yake, diwani Siocha alimtuhumu Dkt Monda kwa ufisadi na matumizi mabaya ya afisi yake.

Shughuli katika Bunge la Kisii ambapo madiwani walijadili hoja ya kumtimua Naibu Gavana wa Kisii Dkt Robert Monda mnamo Februari 29, 2024. PICHA | WYCLIFFE NYABERI

Gavana Arati hajawa na uhusiano mzuri na naibu wake tangu Novemba 2023 wakati Dkt Monda aliwakaribisha nyumbani kwake wakosoaji wa kisiasa wa bosi wake.

Wakosoaji hao ni mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro na Japheth Nyakundi wa Kitutu Chache Kaskazini.

Wengine ni Daniel Manduku (Nyaribari Masaba), Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisii Dorice Aburi na baadhi ya madiwani (MCAs) ambao mnamo Novemba 25, 2023, walikutana na Dkt Monda katika boma lake lililoko kijijini Rigena, eneobunge la Nyaribari Chache. Mkutano huo ulifanyika usiku.

Japo viongozi hao waliwaambia wanahabari kuwa mkutano wao ulikuwa wa kutathmini jinsi ya kufanikisha maendeleo katika kaunti hiyo, ilionekana wazi kwamba viongozi hao walikuwa wakipanga njama kuhusu namna ya kumtenga Gavana Arati dhidi ya viongozi wengine wa kaunti hiyo.

Mkutano huo kwa Dkt Monda ulijiri muda mfupi tu baada ya wanasiasa hao kuhudhuria hafla ya misa katika Kanisa Katoliki la Nyabururu ambapo Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alikuwa mgeni wa heshima

[email protected]