Habari za Kaunti

Madiwani sita wa Murang’a hatarini kusukumwa jela kwa kudaiwa kuzua ghasia

April 28th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MADIWANI sita wa Kaunti ya Murang’a sasa wako katika hatari ya kufungwa jela baada ya kuamrishwa na polisi waandikishe taarifa kuhusu ghasia katika bunge lao.

Nao wanatishia kumfurusha Gavana, Spika na karani wa bunge.

Mnamo Aprili 23, 2024, walifika katika kituo cha polisi kuandikisha taarifa kuhusu kukiuka maadili ya kiuongozi na ambapo sasa wanangojea uamuzi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kuhusu hatima yao mbele ya haki.

Sita hao sasa wanakodolea macho kifungo jela iwapo watashtakiwa na wapatikane na hatia.

Walikuwa wameagizwa kufika katika kituo hicho cha Murang’a na Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kainga Mathiu baada ya kudaiwa walizua fujo katika ukumbi wa bunge lao mnamo Aprili 16, 2024.

Madiwani hao ni Bi Caroline Njoroge wa wadi ya Kigumo, Bw Kenneth Kamau wa Rwathia, Bw Peter Munga (Murarandia), Bw Laban Chomba (Kambiti), Bw Samson Mukora (Kagunduini) na diwani maalum Bi Jane Mukami.

Madiwani hao wameteta kwamba masaibu hayo ni ya kuchochewa kisiasa na Kuna mkono wa mwanasiasa mkuu wa Kaunti hiyo anayetaka kuwathibiti kupitia vitisho.

Hata hivyo, Bw Kainga alisema kinachochunguzwa ni uharibifu wa mali ya umma katika bunge hilo kupitia matendo ya ghasia kinyume na sheria.

Madiwani hao walisema kwamba walikerwa na hatua ya Karani wa Bunge la Kaunti Bw Wilson Kuria na Spika Johnson Mukuha kuonekana kama walikuwa wakihusika katika kukosa kulipwa kwa marupurupu ya madiwani.

Katika mjadala uliozuka, baadhi ya madiwani hao walisema hawakuwa na imani na wenzao wawili ambao ni wanachama wa Bodi ya Huduma ya Umma (PSB).

Wawili hao ni madiwani Bi Wambui Mwangi (Kimorori/Wempa) na Bw Simon Wamwea (Ng’araria) ambao hata walikuwa wametimuliwa kutoka ukumbi wa bunge hilo kupitia hoja ya diwani wa Muguru, Moses Muchiri.

Ni katika mjadala huo uliosemwa kuungwa mkono na madiwani 29 kati ya wote 47 waliokuweko ambapo vurugu zilizuka na kuishia masaibu ya hao sita wanaosemwa kuwa walichangia pakubwa.

Madiwani wengine wamesema kwamba huu ni mwanzo wa ngoma na kuahidi kwamba hivi karibuni wenyeji wa Murang’a watashuhudia hoja za kuwatimua Gavana Irungu Kang’ata na Spika Mukuha.

Wamesema kwamba bunge hilo limejaa ufisadi, mapendeleo na uzembe wa kufanyia wenyeji kazi wengi wakipora tu na wakipigiwa kelele wakome wanazindua misururu ya vitisho wakitumia polisi.

[email protected]