Habari MsetoSiasa

Madiwani walia Joho amekuwa akiwahepa

November 13th, 2019 2 min read

NA MWANDISHI WETU

Kulingana na katiba, gavana anafaa kuhudhuria kikao kimoja cha bunge la kaunti yake kila mwaka kueleza hali ilivyo kimaendeleo na changamoto zilizopo.

Wakiongozwa na diwani wa wadi ya Likoni, Bw Athman Mwamiri, MCA hao walimtaka kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti hiyo, Bw Hamisi Musa kuelezea sababu za gavana wao kukosa kuhudhuria kikao mwaka huu.

Bw Musa ambaye ni diwani wa Mtongwe alisema: ‘Gavana wetu Joho anafaa kuhudhuria kikao kimoja cha bunge kila mwaka, na kwa vile amewahi kuhudhuria kikao cha mwaka huu, anatarajiwa kuhudhuria kikao cha mwaka ujao hapo Februari.’

Lakini Bw Musa hakufafanua ni kikao kipi ambacho Bw Joho amehudhuria mwaka huu.Diwani wa Wadi ya Tudor, Bw Tobias Samba alimfokea Bw Musa akimuuliza: ‘Ni vipi Gavana atakuja mwaka ujao na mwaka huu hajafika katika kikao cha bunge?’

Hapo Bw Musa aliomba apewe wiki mbili kufuatilia suala hilo, ili awajulishe ni lini gavana alihudhuria kikao cha mwaka huu na ni lini atafika kikao cha mwaka ujao.

Naye Bw Mwamiri alisema Gavana Joho anafaa atoe ripoti ya mapema kwani mwaka unakaribia kuisha.’Hilo analosema Bw Musa haliwezekani. Kama Gavana atakuja mwaka ujao katika kikao basi itakuwa mwaka wa pili bila ya kumuona gavana hapa kikaoni,’ akasema Bw Mwamiri.

Msemaji wa gavana huyo Richard Chacha alisema Bw Joho tayari amehudhuria kikao cha mwaka huu lakini hakusema ni lini alihudhuria kikao hicho akiahidi kueleza baada ya kuthibitisha.Bw Joho ameonekana mara kadha kwenye mitandao ya kijamii akijivinjari ng’ambo.

Mienendo yake tangu aliposhinda ugavana kwa mara ya pili mnamo 2017 umewafanya baadhi ya wakazi wa Mombasa wafikirie amejitenga nao, kinyume na alivyokuwa wakati wa muhula wake wa kwanza.

Wakati wa Mashujaa Dei, wakazi wa Mombasa walimsubiri kwa hamu awatetee kuhusu hali ya uchumi wa kaunti hiyo lakini aliwaacha midomo wazi aliposema kuwa hatasema lolote kuhusu SGR kupewa kibali cha kubeba makasha kutoka bandarini.