Habari MsetoSiasa

Madiwani waliosema Joho ni mfisadi watimuliwa

July 22nd, 2020 2 min read

Na FARHIYA HUSSEIN

MADIWANI wa Kaunti ya Mombasa ambao walimshtaki Gavana Hassan Joho kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa madai ya utumizi mbaya ya fedha za umma, wameadhibiwa kwa kutupwa nje ya Kamati za Bunge.

Akiongea na Taifa Leo jana, diwani wa Jomvu Kuu, Athman Shebe, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira, alithibitisha kuwa yeye ni mmoja wa walioondolewa katika kamati za bunge.

‘Tulitolewa kwa sababu tulijitokeza wazi kuzungumzia jinsi fedha za umma zinavyotumika na serikali ya kaunti, ‘akasema Bw Shebe.

Mwakilishi mwingine ambaye alipata pigo ni Charles Kitula wa wadi ya Freretown, ambaye alikuwa kiranja wa wengi katika bunge la kaunti: ‘Tumeondolewa kwenye kamati zote za bunge bila kupewa taarifa yoyote,’ akasema Bw Kitula.

Mwenzake wa wadi ya Kongowea, Abrari Omar naye alisema imekuwa shida kubwa kwao kuwasilisha hoja yoyote bungeni.

“Kamati ya biashara bungeni inaendeshwa na washirika wa gavana. Lakini tumeamua hatutakaa kimya tena. Tutatumia njia zote za kisheria kwani tuna ushahidi wote unaohitajika kumuondoa gavana wa kaunti yetu madarakani,’ Bw Omar alisema.

Diwani mmoja aliambia Taifa Leo kuwa walifanya mkutano mnamo Jumatatu ndani ya majengo ya bunge kuamua adhabu kwa madiwani wanaomkosoa Bw Joho’Mkutano wa madiwani wa ODM ulifanyika kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka mitatu iliyopita mnamo Jumatatu.

Kusudi kuu lilikuwa kujadili jinsi wawakilishi wa wadi wanaozunguka wakimshutumu gavana wa kaunti wataadhibiwa,’ alisema diwani ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya fedha katika bunge la kaunti, Bw Mohammed Hatimy alipinga madai ya madiwani wanaomlaumu Bw Joho akisema hayana msingi.

Mnamo Jumanne, Mkuu wa EACC eneo la Mombasa, Bw Mutembei Nyaga alithibitisha kuwa amepokea ripoti kutoka kwa madiwani kuhusu madai ya matumizi mabaya ya pesa katika kaunti hiyo.

Bw Nyaga alisema EACC itaamua hatua za kuchukua baada ya kuchunguza madai yaliyowasilishwa, ambayo yanahusu utumiaji mbaya wa takribani Sh30 bilioni zilizokuwa kwenye bajeti ya kaunti tangu 2017.