HabariSiasa

Madiwani wapewe mamlaka ya kuchunguza magavana – Murkomen

April 24th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa wengi katika seneti Kipchumba Murkomen, Jumanne aliwachangamsha madiwani wanaohudhuria Kongamano la Ugatuzi mjini Kakamega, kwa kuwataka magavana kukubali utendakazi wao uchunguzwe.

Bw  Murkomen alisema madiwani wapaswa kuruhusiwa kufanya kazi yao ya kuhakikisha pesa za umma zinatumiwa vyema.

“Tulianza ugatuzi baada ya uchaguzi mkuu wa 2013 kwa mizozo na makabiliano badala  ya mashauriano na ushirikiano. Kongamano hili linafaa kufungua ukurasa mpya wa serikali  ya kitaifa, serikali za kaunti na wadau wote kufanyakazi pamoja,” alisema Bw Murkomen.

Alisikitika kuwa ugatuzi umetatizwa na wanaofikiria kuwa mfumo huo unahusu magavana pekee.“Ugatuzi ni mfumo muhimu kuliko magavana, madiwanmi na hata serikali ya kitaifa,” alisema.

Aliwalaumu magavana kwa kuhujumu wanaopaswa kupiga msasa utendakazi wao.

“Magavana waachie madiwani nafasi ya kutekeleza majukumu  yao,’ alisema huku akishangiliwa na madiwani.

Aidha, aliwashutumu magavana kwa kuwadharau manaibu wao na kukataa kuwapa majukumu ya kutekeleza.

“Siku hizi, manaibu wa magavana wamebadilishwa kuwa wasomaji wa magazeti. Kila mmoja anafaa kuhisi kwamba anatoa mchango wa kuendeleza nchi,” alisema.

Alisema seneti itashughulikia mswada wa kutaka kubuniwe hazina za wadi zitakazosimamiwa na madiwani ili kuhakikisha unatimiza mahitaji yote ya katiba.

“Madiwani walipokuwa wakifanya kampeni, waliahidi maendeleo na hazina hizo zitawasaidia kutimiza ahadi hizo na kupeleka pesa mashinani zaidi,” alisema.