Habari Mseto

Madiwani wapunjwa na 'kamanda wa polisi'

April 17th, 2018 1 min read

Na BRUHAN MAKONG

Wawakilishi sita wa Kaunti ya Wajir wametapeliwa na mhalifu aliyejifanya kamanda wa polisi wa kaunti hiyo Bw Stephen Ng’etich.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Ng’etich alisema mwanamume huyo aliwapigia simu madiwani hao kwa kutumia nambari 0723475525.

Aliwadanganya kuwa yeye (kama kamanda) alikuwa ameamua kuwapa silaha madiwani hao kwa Sh20,000 kila mmoja kwa sababu ya kudhoofika kwa usalama eneo hilo.

Tapeli huyo aliwataka kuharakisha kulipa ada hiyo akidai bunduki zilizokuwa zimesalia zilikuwa chache mno.

Aliwapa wawakilishi hao nambari ya MPESA, 0722858786, ambayo wawakilishi hao sita walifaa kutuma pesa hizo. Lakini hawakuwa na bahati kwani walipoteza pesa hizo.

Kulingana na ujumbe wa MPESA, nambari hiyo ilisajiliwa chini ya jina John Njoroge Githua. Kamanda huyo alisema  uchunguzi kuhusu suala hilo umeanzishwa.