Habari Mseto

Madiwani wasuka tena mpango wa kumtimua Kawira

April 22nd, 2024 1 min read

Na DAVID MUCHUI

MASAIBU ya Gavana wa Meru, Kawira Mwangaza yanaendelea huku madiwani wakipanga jaribio la nne la kumbandua baada ya kugonga mwamba mara tatu.

Bi Mwangaza alikabiliwa na hoja ya kung’olewa ofisini mara ya kwanza 2022, takriban miezi minne baada ya kuapishwa kabla ya kupata nafuu kortini kwa kuwa madiwani hawakuwa wameshirikisha umma.

Hata hivyo, alibanduliwa baadaye kabla ya kuokolewa na Seneti mnamo Desemba 2022. Miezi 10 baadaye, madiwani waliwasilisha hoja nyingine lakini uamuzi wao ukabatilishwa na Seneti Novemba 2023.

Akizungumza Jumamosi wakati wa mazishi ya watoto wa Naibu Spika Mwenda Ali waliofariki katika ajali ya barabarani, diwani maalum Secondina Kanini alifichua kuwa wataandaa hoja nyingine ya kumfurusha kutoka ofisini.

“Tunachotaka ni kuungwa mkono na watu wa Meru kwa sababu hivi karibuni tutaelekea Seneti. Wakati huu, viongozi wanawake watakuwa mstari wa mbele kumbandua gavana. Kama atalia, pia sisi tutalia,” Bi Kanini alisema.