Madiwani wataka kupewa bunduki ‘kupambana’ na polisi

Madiwani wataka kupewa bunduki ‘kupambana’ na polisi

Na FLORAH KOECH

MADIWANI wa Kaunti ya Baringo wanataka serikali iwape walinzi au kuwapa idhini ya kumiliki bunduki kama njia ya kujilinda dhidi ya polisi.

Katika mjadala uliowasilishwa bungeni Jumatano, madiwani hao walidai kuwa serikali inawalenga kwa kupinga mchakato wa maridhiano wa BBI uliotupiliwa mbali na korti wiki jana.

Walisema kuwa na walinzi ama kupewa idhini ya kumiliki bunduki ni njia ya kuwalinda dhidi ya dhuluma za polisi.

Walidai usalama wao uko hatarini hasa baada ya polisi waliojihami kufika katika eneo la bunge Jumatano bila kufahamu nia waliokuwa nayo.

Wawakilishi wa wadi hao walidai serikali sharti izingatie usalama yao hasa baada ya mmoja wao kutekwa nyara mwaka wa 2017 na watu waliodaiwa kuwa polisi na mwili wake kupatikana Oldonyo Sabuk kaunti ya Machakos siku chache.

Mwakilishi wadi wa Bartabwa, Reuben Chepsongol, alidai kuwa yeye na mwenzake Silas Tochim (wadi ya Tenges) walikuwa walengwa wakuu baada ya kushutumu maafisa wa serikali.

“Usalama wa madiwani wa Kaunti ya Baringo uko hatarini. Tulishangaa sana kuwapata maafisa wa polisi waliojihami wamejaa nje ya bunge. Ikiwa suala hili halitashughulikiwa, tutachukua hatua,” akasema Bw Chepsongol.

Alisema kesi za utekaji nyara zimeongezeka katika eneo hilo hasa uchaguzi mkuu wa mwaka ujao ukikaribia.

“Tunashuku kuna wanasiasa ambao wanawatumia maafisa wa polisi ili kutushtua,” akaongeza Bw Chepsongol.

Alisema serikali lazima iangazie suala la usalama wao.

“Tunashangaa ni kwa nini polisi hao walifika katika eneo la bunge na hakukuwa na maandamano yoyote. Hali hii inatuweka hatarini hasa jinsi wengine wetu tulivyokataa kuunga mkono itikadi mbalimbali zilizowekwa na serikali ikiwemo BBI,” akasema Bw Chepsongol.

Kwa upande wake, Bw Tochim alidai wanasisa wengine wanajaribu tu kuwatishia madiwani ili wauunge mkono BBI.

“Inakuaje polisi wanaofaa kutulinda wamekuja wakiwa wamejihami tukijadili mchakato wa BBI. Kwa sababu hiyo, tunafaa kupewa walinzi ama idhini ya kumiliki bunduki,” akasema Bw Tochim.

Naibu spika Jacob Cheboiwo alishangazwa na tukio hilo na hata kuitaka serikali kuwaeleza shida iliyo kati yao.

“Tunaamini kuwa polisi hao wanatumiwa vibaya na wanasisa wengine serikalini ili kuwaunga mkono. Hatutashtuliwa na tukio hilo. Tutaendelea kusimama kidete kimaamuzi,” akasema Bw Cheboiwo.

You can share this post!

Hofu msongamano wa chanjo huenda uibue maambukizi

Mtihani mgumu kwa Arsenal ugenini Etihad