Habari MsetoSiasa

Madiwani wataka uchunguzi kuhusu maiti ya paka bungeni

September 11th, 2018 1 min read

Na STEPHEN ODUOR

WANACHAMA wa Bunge la Kaunti ya Tana River wanaitaka afisi ya karani wa bunge hilo kutoa picha za kamera za CCTV na ripoti kuhusu paka mmoja aliyepatikana amefariki katika majengo ya bunge hilo Agosti 22 mwaka huu.

Kwenye taarifa aliyoitoa katika bunge hilo Jumanne, kiongozi wa wengi Salah Afamop alisema suala hilo linapasa kuchukuliwa kwa uzito zaidi.

Alisema uchunguzi wa kina unafaa kuendeshwa kubaini jinsi paka huyo aliingia katika afisi ya karani, jinsi na kwa nini aliuawa.

“Mheshimiwa Spika, suala hilo halifai kuchukuliwa kwa urahisi kwani limesababisha wasiwasi miongoni mwa wananchi. Tunahitaji maelezo kamili na picha za CCTV kuhusu kilichotendeka,” akasema.

Bw Adamo alisema madiwani wanafaa kuhakikishiwa usalama wakati maelezo kuhusu tukio hilo yatakapotelewa.

Kulingana na Diwani huyo kuuawa kwa paka ndani ya afisi ya karani inaweza kusababisha woga na wasiwasi.

“Tukio linaweza kuwa ajali, lakini pia kinaweza kutumia kutoa ujumbe kwa mtu fulani ambayo inaweza kuashiria jambo lingine lisilo la kawaida,” akasema.

Diwani huyo aliwaka wafanyakazi katika bunge hilo kuelezea jinsi paka huyo aliiingia ndani ya afisi hiyo ambaye madirisha yake yamewekwa nyaya na huwa inafungwa kila mara. Pia walitaka kujua idadi ya paka hao kwani wanyama hao huwa hawafugwi katika majengo ya bunge hilo.

Alisema tukio hilo linaashiria kuwa wafanyakazi wa bunge hilo wamekuwa wazembe katika majukumu yao, kwani lilidhihirisha kuwa mtu fulani anaweza kuingia katika majengo ya bunge hilo na kuteka vilipuzi bila kugunduliwa.

“Ikiwa mnyama anaweza kuingia katika majengo ambayo yana ulinzi mkali, basi kuna uwezekano kwamba mtu anaweza pia kuingia na kuteka vilipuzi au bomu bila kujulikna. Hali hii ni hatari kwa maisha ya waheshima madiwani na wahudumu wengine katika bunge hili,” akasema.