Habari Mseto

Madiwani wataka vituo vya kansa katika hospitali zote Nairobi

July 22nd, 2019 1 min read

Na Collins Omullo

MADIWANI katika Kaunti ya Nairobi wamehimiza uongozi wa kaunti hiyo kuanzisha vituo vya kupima na kuchunguza maradhi ya saratani kwenye hospitali na vituo vyake vya afya.

Kulingana nao, vituo hivyo vitasaidia raia kugundua mapema iwapo wanaugua saratani kisha kutafuta matibabu na kuzuia vifo.

Diwani wa Karura, Bw Joseph Wambugu ambaye aliwasilisha mswada wa kuanzisha vituo hivyo wiki jana, alisema njia pekee ya kupambana na kansa ni mgonjwa kupata matibabu kabla maradhi hayo kuenea na kufikia kiwango hatari.

“Tunaiomba serikali ya kaunti kuanzisha vituo vya kuchunguza saratani na njia ya kuzuia maradhi haya hatari. Vituo vya VCT vilisaidia pakubwa katika kupunguza maambukizi ya maradhi ya Ukimwi,” akasema Bw Wambugu.

Kiongozi huyo alisema saratani imepanda hadi nafasi ya tatu kati ya maradhi hatari yanayosababisha vifo nchini na akaongeza kwamba Shirika la Afya Duniani(WHO) lilifichua kwamba watu 37,000 hupata maradhi hayo kila mwaka na wengine 28,000 pia wakifariki.