Madiwani wavuna baada ya SRC kuidhinisha kila mmoja apewe Sh2 milioni za gari

Madiwani wavuna baada ya SRC kuidhinisha kila mmoja apewe Sh2 milioni za gari

Na CHARLES WASONGA

TUME ya Mishahara na Marupurupu (SRC) imeidhinisha ruzuku Sh4.5 bilioni za kununua magari kwa madiwani wote 2,224 nchini kama ilivyopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta juzi.

Kwenye taarifa, Mwenyekiti wa tume hiyo Lyn Mengich alisema hatua hiyo itachangia kila mmoja wa madiwano kupokea Sh2 milioni za kununulia magari.

Alisema SRC imefikia uamuzi huo kutokana na hali ya kuimaridha “haki na usawa.”

Katika taarifa hiyo ambayo nakala yake ilitumiwa Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Martin Wambora, Bi Mengich alisema kuwa maspika wote wa mabunge ya kaunti na madiwani ambao walikuwa wamechukua mikopo ya kununua magari sasa watapata afueni kwani mikopo hiyo itageuzwa kuwa ruzuku.

Kando na ahadi kuhusu ruzuku hiyo iliyotolewa juzi na Rais Kenyatta alipokutana na madiwani kutoka kaunti za Mlima Kenya katika Ikulu ndogo ya Sagana, Bw Wambora pia alikuwa amewasilisha ombi hilo kwa SRC.

Mwenyekiti wa Muungano wa Maspika wa mabunge ya kaunti Ndegwa Wahome alipongeza hatua ya madiwani kupewa ruzuku ya kununua magari akisema itaimarisha uwezo wao wa kufuatilia kwa makini utekelezaji wa ugatuzi.

Madiwani wamekuwa wakiendesha kampeni ya kutaka wapewe ruzuku ya kununua magari wakati huu wa mjadala kuhusu mageuzi ya Katiba ya BBI.

6,000 kati yao waliokutana na Rais Kenyatta katika Ikulu ya Sagana, walitaka wapewe pesa ili waunge mkono mswada wa BBI.

Naye kiongozi wa ODM Raila Odinga alipokutana na madiwani kutoka Nyanza katika hoteli moja eneo la Karen, Nairobi, aliunga mkono pendekezo hilo akisema “madiwani wana haki ya kupata manufaa hayo.”

“Nawahikikisha kuwa Rais atatimiza ahadi hii kwa sababu ninyi kama madiwani ndio mwatekeleza wajibu muhimu wa kukutana na wananchi katika ngazi ya mashinani mkiwafanyia kazi,” akasema Bw Odinga.

Lakini wandani wa Naibu Rais William Ruto wametaja hatua hiyo kama kuwahonga madiwani ili wapitishe mswada wa BBI.

Tayari mabunge ya Siaya na Kisumu yamepitisha mswada huo ambao unalenga kubadilisha muundo wa uongozi serikalini.

Kulingana na Katiba, angalau mabunge 24 yanahitajika kuupitisha mswada huo kabla ya kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa na Seneti kujadiliwa kabla ya kura ya maamuzi kufanyika.

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Uzuri na ubaya wa mtu umo ndani ya mtu...

AFROBASKET: Kenya Morans yalenga kumaliza ukame wa miaka 28