Madiwani zaidi ya 50 Murang’a waelezea kuunga BBI

Madiwani zaidi ya 50 Murang’a waelezea kuunga BBI

Na LAWRENCE ONGARO

MADIWANI – MCAs – wapatao 50 kutoka Kaunti ya Murang’a wamesema kwa kauli moja kuwa mswada wa BBI ukiletwa katika bunge la kaunti wataupitisha mara moja bila kuchelewa.

Wakiongozwa na kiongozi wa wengi Bw Eric Kamande, walisema umefika wakati wa kubainisha mbivu na mbichi.

“Sisi madiwanitunaingoja mswada huo kwa hamu ili tuipitishe haraka iwezekanavyo. Wakati huu tunataka kuingia mashinani ili tuzungumze na wananchi kwa upole na unyenyekevu,” alisema Bw Kamande.

Aidha, walisema kuwa wanataka kuhakikisha Kaunti ya Murang’a inakuwa ya kwanza kuikubali BBI.

“Hatutakubali kupewa porojo sisi jamii ya watu kutoka Mlima Kenya. Sisi pia in lazima tuwe na usemi katika serikali ijayo ya 2022,” alisema Bw Kamande.

Mkutano huo ulioendeshwa katika hoteli moja mjini Thika, mnamo Alhamisi, uliendelea kwa muda wa saa nane kabla ya kukamilika.

Gavana wa Murang’a Bw Mwangi Wa Iria aliyeongoza hafla hiyo alisema watahakikisha eneo la Mlima Kenya haligeuzwi “uwanja wa kujitakia makuu.”

“Sisi kama Jamii ya Mlima Kenya tunastahili kujipanga kwa kuhakikisha tunakuwa kitu kimoja. Hatutaki watu wanaotaka kutugawanya katika makundi mawili,” alisema Bw Wa Iria.

Alisema viongozi wa Mlima Kenya watalazimika kuja pamoja na kuzungumza kwa sauti moja.

Gavana huyo alisema hata yeye yupo katika kinyang’anyiro cha urais huku akitarajia kutumia chama cha ‘Usawa Kwa Wote’.

“Nitazunguka katika eneo la Kati na maeneo mengine kutafuta kura. Kila mmoja ana haki ya kufanya kampeni na kutafuta kura popote pale katika nchi hii,” alisema.

Alichukua zaidi ya muda wa saa tatu kueleza kuhusu mazuri yaliyomo katika Mswada wa marekebisho ya katiba kupitia BBI.

Alisema eneo la Mlima Kenya halitakubali kumuaibisha Rais Uhuru Kenyatta “nyumbani kwake.”

“Tutafanya juu chini kama viongozi kuona ya kwamba Rais Kenyatta anakamilisha ajenda muhimu alizoahidi kabla ya wakati wake wa kustaafu kuwadia.

Alisema mikakati walioweka kuvumisha ripoti ya BBI ni kuhakikisha viongozi wote wa zamani wanajumishwa katika kamati ya kuhamasisha kuhusu BBI.

Aidha, alisema washika dau wote watajumuishwa katika mpango huo.

You can share this post!

Motisha tele kambini mwa Kenya Morans baada ya mwanavikapu...

Okutoyi achafua Safi na kutinga fainali tenisi ya World...