Habari Mseto

Maduka ya jumla yanavyhakikisha wateja hawakaribiani

April 17th, 2020 2 min read

NA SAMMY WAWERU

Uzingatiaji wa umbali baina ya mtu na mwenzake ni miongoni mwa vigezo wanavyopaswa kuzingatia watu wakiwa maeneo ya umma, ili kuzuia maambukizi ya Covid – 19.

Wizara ya Afya imependekeza unapotangamana na mtu, uwe umbali usiopungua mita moja.

Hata hivyo, ni kigezo ambacho kimeonekana kuwa na ugumu kutekelezwa, kwa kile kinachotajwa kama “utepetevu na watu kupuuza”.

Licha ya matawi ya maduka ya kijumla ya Powerstar kukiri kupitia changamoto kuhakikisha wateja wanazingatia agizo hilo, kwenye sakafu yamewaelekeza kupitia michoro ya umbali kati ya mtu na mwenzake.

Michoro inayoelekeza kwa njia ya makanyagio, inamtaka kila mteja asimame mita moja na nusu mbali na mwenzake, hususan kwenye foleni kulipia bidhaa. “Yanasaidia kupunguza msongamano kwenye laini. Hata hivyo, haijakuwa rahisi kwetu kuhimiza wateja,” Ann Njoki ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa Powerstar tawi la Zimmerman, Nairobi, akaambia Taifa Leo Dijitali.

Njoki alisema mikakati waliyoweka kudhibiti usambaaji wa virusi vya corona, inatekelezwa katika matawi ya maduka yote ya Powerstar.

Katika tawi la Zimmerman, wateja wanatakiwa kunawa mikono kwa maji na jeli, yaliyowekwa mlangoni, sehemu ya nje kabla ya kuingia. Pia, kuna vitakasa mikono. “Tunatilia maanani wateja wavalie maski,” Njoki akasema.

Taswira hiyo pia inawiana na ya maduka ya kijumla ya Naivas, ambapo yanapima kiwango cha joto cha kila mteja kabla kuruhusiwa kuingia. “Kiwango cha joto kikipita nyuzi 37 haturuhusu huyo mteja kuingia,” mhudumu mmoja anayetekeleza shughuli hiyo Naivas tawi la Githurai akaeleza, ingawa hakufichua hatua wanayochukulia mhusika – mteja ambaye kiwango chake cha joto mwilini kinazidi kile cha kawaida.

Virusi vya corona ni kundi kubwa la virusi ambavyo vinaweza kusababisha magonjwa kuanzia homa ya kawaida kwenda kwa magonjwa mazito ya kupumua kama pumu, nimonia au ugonjwa kali wa kupumua kwa papo hapo (SARS).

Dalili ya aliyeambukizwa virusi hivyo ni homa, kikohozi, ugumu wa kupumua, kiwango cha joto mwilini kupita kile cha kadri, miongoni mwa zingine.

Maduka ya kijumla ya Naivas pia yanadhibiti kiwango cha wateja wanaoingia mara moja. “Wateja wanapanga laini, ili kudhibiti msongamano ndani ya duka,” mlinzi mmoja wa Naivas tawi la Allsoaps, Nairobi, akasema.

Maduka ya kijumla na benki, ni miongoni mwa maeneo yanayopokea idadi kubwa ya watu. Masoko ya bidhaa za kula pia yanashuhudia idadi kuu ya wateja.