Habari Mseto

Maelezo ya polisi jinsi wakili Kimani aliuawa yakubaliwa kama ushahidi

September 18th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu Jumatano ilitupulia mbali ombi la kachero anayeshtakiwa pamoja na maafisa wanne wa polisi wa utawala kwa mauaji ya wakili Willie Kimani na watu wengine wawili.

Jaji Jessie Lesiit alitupilia mbali ombi la Peter Ngugi Kamau almaarufu Brown la kutaka maungamo yake jinsi Bw Kimani na wenzake walivyouawa yatupwe.

Na wakati huo huo Jaji Lesiit aliamuru mashahidi wawili waliokuwa wametoa ushahidi hapo awali wafike tena mahakamani kukariri jinsi walisema.

Jaji huyo alimruhusu wakili Katwa Kigen kumwakilisha Konstebo Sylvia Wanjiku anayeshtakiwa pamoja na Fredrick Leliman, Stephen Cheburet na Leonard Maina Mwangi.

Washtakiwa wote watano wakiwa kizimbani. Picha/ Richard Munguti

Wote watano wamekanusha mashtaka ya kuwaua Willie Kimani , mteja wake Josephat Mwenda na Joseph Muiruri.

Kimani, Mwenda na Muiruri walitekwa nyara wakitoka mahakama ya Mavoko kaunti ya Machakos mnamo Juni 23 2016.

Katika taarifa by kurasa 21 iliyonukuliwa na Inspekta Geoffrey Kinyua mshtakiwa alikariri kwa undani jinsi maafisa hao wa polisi waliwazuilia wahasiriwa katika kituo cha polisi cha Syokimau, wakawatoa usiku na kuwaua kisha wakatupa maiti zao katika mto Athi River karibu na eneo la Donyo Sabuku.

Maiti za watatu hao zilipatikana baada ya siku saba kama zimeoza.

Wakili Katwa Kigen azugumza na mshukiwa Sylvia Wanjiku. Picha/ Richard Munguti

Ushahidi uliotolewa mahakamani ulisema vichwa vya watatu hao zilikuwa zimefishwa makaratasi ya Mulley Supermarket. Maiti zao zilikuwa zimewekwa ndani ya magunia.

Mawimbi ya kifaa cha mawasiliano ya polisi (walkie Talkie) alichokuwa nacho Leliman yaliandamwa kutoka Syokimau hadi mto Athi.

Maiti zilisafirishwa kwa gari la Lelimani usiku wa Juni 23/24, 2016. Kiongozi wa mashtaka ni naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma Bw Nicholas Muteti.

Jaji Lesiit aliamuru kesi iendelee Oktoba 7,2019