Maelfu katika hatari ya kufa kwa corona

Maelfu katika hatari ya kufa kwa corona

Na BENSON MATHEKA

MAELFU ya Wakenya wako katika hatari kubwa ya kufariki katika wimbi la tatu la Covid-19 kutokana na aina mpya ya virusi kutoka Uingereza, Afrika Kusini na Brazil.

Hatari hii inaongezeka zaidi kwa Wakenya kutokana na gharama za juu za matibabu katika hospitali za kibinafsi na huduma duni za afya ya umma nchini.

Pia wizi wa pesa za kukabiliana na Covid-19 mwaka 2020 kupitia KEMSA umeweka maisha ya Wakenya katika hatari kuu.

Hospitali nyingi zilizo na vitanda vya wagonjwa mahututi (ICU) zimeongeza bei kwa hadi mara tatu ya inayotozwa wanaougua maradhi mengine.

Uchunguzi wa Taifa Leo umeonyesha kuwa hospitali nyingi zinaitisha amana ya juu zaidi kabla ya mgonjwa wa Covid kukubaliwa kuingizwa ICU.

Hospitali za Nairobi Hospital na Mater jijini Nairobi zinatoza amana ya Sh600,000 huku ile ya kitaifa ya Kenyatta (KNH) ikidai Sh200,000.

Kulingana na daktari mmoja ambaye aliomba tusitaje jina lake, kuna baadhi ya hospitali jijini Nairobi zinazoitisha amana ya hadi Sh1 milioni.

Pesa hizi ni sehemu ya kwanza tu ya gharama, kwani zinaongezeka kwa Sh52,000 kila siku, ambayo ni ada za kuhudumia wagonjwa wa Covid walio ICU kulingana na mwongozo wa Taasisi ya Utafiti wa Matibabu (KEMRI) iliyotolewa mwaka 2020.

“Hali ikiendelea hivi, ugonjwa huu utaua maelfu. Ebu jiulize ni Wakenya wangapi wanaoweza kulipa Sh1 milioni kupata kitanda cha ICU? Ikizingatiwa kasi na hatari ya maambukizi, maskini wengi, wakiwemo wahudumu wa afya wataangamia kwa wingi,” alisema daktari wa hospitali moja katika Kaunti ya Machakos aliyeomba tubane jina lake.

Hali imegeuka kuwa mbaya zaidi kutokana na uhaba wa vitanda vya ICU, ambapo asilimia 87 ya jumla ya 518 vilivyoko nchini kwa sasa vina wagonjwa.

Hii ina maana kuwa wengi wa wagonjwa ambao wamo katika hali mahututi wamo kwenye hatari ya kufariki kutokana na kushindwa kumudu gharama ya amana na ada za ICU, pamoja na kukosekana kwa vitanda hivyo.

Mashambani

Hii imetokea wakati ambapo maambukizi nchini yamefikia kiwango cha juu huku idadi ya wanaofariki nayo pia ikipanda.

Taasisi ya Matibabu ya Amerika (CDC) imeorodhesha Kenya katika ngazi ya nne, ambayo ina maana kuwa nchi imo na maambukizi ya kiwango cha juu zaidi.

Hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya mashambani kutokana na huduma duni katika hospitali nyingi. Hii inawaacha wakazi wa mashambani, ambako umaskini uko juu zaidi, katika hatari zaidi ya kufariki kutokana na makali ya Covid-19.

Mnamo Jumatatu, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alionya kuwa kuwa hospitali zinalemewa na wagonjwa kufuatia wimbi la tatu la maambukizi ya corona.

Madaktari wanasema ukosefu wa vitanda vya wagonjwa mahututi na oksijeni katika hospitali za umma unasababisha vifo vya wagonjwa wengi wanaombukizwa virusi hivyo.

Wataalamu wa afya wanahofia kuwa wagonjwa wengi wa corona wanafariki wakiwa nyumbani bila kujua wanaugua.

Pia uhaba wa kemikali za kupima virusi vya Covid-19 una maana wengi hawajui wanaugua.

Hali hii imeibuka ikigunduliwa kuwa kaunti nyingi hazikuweka vitanda 300 kila moja katika maeneo ya kutenga wanaoambukizwa virusi vya corona kama zilivyoagizwa na Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2020.

Pia imeibuka hospitali nyingi mashinani hazina vitanda vya ICU. Wiki iliyopita, mwanahabari katika Kaunti ya Embu aliyekuwa hali mahututi, alikosa kitanda na ikabidi apelekwe kaunti jirani ya Murang’a.

Madaktari nao wanahofia kuwa jinsi maambukizi yanavyoongezeka ndivyo nao wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa corona wakiwa kazini.

“Kila mtu yumo kwenye hatari. Hili wimbi la tatu ni hatari zaidi kwa sababu ya uhaba wa vifaa na vyumba vya kutibu na kutenga wagonjwa,” asema daktari katika KNH.

Hali hii inapotokea, watu waliofaidika na mabilioni ya pesa za kushughulikia janga la corona bado hawajachukuliwa hatua, licha ya Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2020 kuagiza wakamatwe na washtakiwe.

Zaidi ya Sh7.6 bilioni zililipwa watu na kampuni zilizopata tenda ya kuuzia serikali vifaa vya kujikinga na corona kupitia Shirika la Kusambaza Dawa la Kenya (KEMSA).

Pia kuna hofu kwamba baadhi ya pesa zilipewa kaunti kujiandaa kukabili janga la corona zilitumiwa vibaya.

You can share this post!

KINA CHA FIKRA: Daima Magufuli atakumbukwa kwa uzalendo na...

KAULI YA MATUNDURA: Mshabaha kati ya Rais Magufuli na...