Maelfu kuenda Uingereza kabla ya marufuku kuanza

Maelfu kuenda Uingereza kabla ya marufuku kuanza

Na LEONARD ONYANGO

SHIRIKA la Ndege la Kenya (KQ) limeongeza idadi ya ndege zitakazohudumia idadi kubwa ya watu wanaotaka kwenda Uingereza kabla ya marufuku ya kuzuia abiria kutoka Kenya kuanza kutekelezwa Ijumaa, wiki hii.

Kampuni ya KQ ilitoa tangazo hilo saa chache baada ya Kenya kulipiza kisasi kwa kutangaza kuwa kuanzia Ijumaa, Aprili 9, abiria wote wanaowasili humu nchini kutoka Uingereza watawekwa karantini kwa siku 14.

Serikali, kupitia taarifa yake iliyotolewa na wizara ya Mashauri ya Kigeni, ilisema kuwa wasafiri kutoka Uingereza watajilipia gharama ya kuwekwa karantini.

Serikali ilikerwa na hatua ya Uingereza kuingiza Kenya kwenye orodha ya mataifa yaliyo na maambukizi tele ya virusi vya corona licha ya juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa kukabiliana na maradhi hayo.

“Kenya imeweka juhudi na bidii nyingi katika kukabiliana na janga la virusi vya corona. Kenya imepongezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutokana na juhudi zetu kupambana na virusi vya corona,” ikasema taarifa ya wizara ya Mashauri ya Kigeni.

Uingereza ilipiga marufuku wasafiri kutoka Kenya kuingia katika nchi hiyo ya Ulaya baada ya idadi kubwa ya abiria kupatikana na aina ya virusi vya corona ya B.1.351, vilivyogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini.

Kulingana na Uingereza, asilimia 70 ya abiria kutoka Kenya wanaopatikana na virusi vya corona wana aina ya B.1.351.

Marufuku hiyo ni pigo kwa Kenya kwani wasafiri wengi wamekuwa wakipitia Nairobi kuelekea Uingereza baada ya Afrika Kusini, Ethiopia, Qatar na Miliki za Uarabuni (UAE) kuingizwa kwenye orodha hiyo nyekundu mwaka jana.

Nchi nyingine za Afrika Mashariki zilizoko kwenye ‘orodha nyekundu’ ya Uingereza ni Tanzania, Burundi na Rwanda.

Shirika la KQ jana lilisema kuwa limeongeza ndege mbili ili kuhudumia idadi kubwa ya abiria wanaotaka kuelekea Uingereza kabla ya marufuku kuanza kutekelezwa Aprili 9.

“Watu waliokuwa wamelipia tiketi za kutaka kwenda Uingereza baada ya Aprili 9, watarejeshewa fedha zao au watazitumia baada ya marufuku hiyo kuondolewa,” ikasema KQ.

You can share this post!

Jenerali Badi awaangushia shoka maafisa 13 wa NMS

Kivumbi kikali chaja, wandani wa Gideon waonya mahasimu