Habari za Kitaifa

Maelfu waachwa bila ajira Remotasks ikisimamisha shughuli zake Kenya

March 16th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

KAMPUNI maarufu ya kutoa kazi za uandishi za mitandaoni, Remotasks, imesimamisha shughuli zake nchini Kenya.

Taifa Leo imebaini kwamba kampuni hiyo ilituma barua pepe kwa wafanyakazi wake kwamba imesimamisha shughulli zake nchini, ijapokuwa haikutoa  sababu zozote.

“Tumesimamisha shughuli zetu katika eneo lako kuanzia Machi 8, 2024. Kutokana na mabadiliko hayo, hutaweza kuingia katika jukwaa hili. Utapata malipo yako kuhusiana na kazi uliyofanya kupitia akaunti yako ulijisajilisha nayo,” ikaeleza barua pepe hiyo.

Mamia ya wafanyakazi wake walieleza mahangaiko yao, baada ya kupata ujumbe wa kuwazuia kuigia kwenye tovuti yake.

Walisema walipata ujumbe wa uliowaambia: “Pole, umezuiwa kuingia katika jukwaa hili.”

Remotasks ni jukwaa la mtandaoni ambalo hutoa nafasi kwa waatumizi wake kupata pesa kupita shughuli kama uandishi, uwekaji data katika majukwaa tofauti kati yaa mengine.

Kufungwa kwa kampuni hiyo, yenye makao yake nchini Amerika, kumewaacha vijana wengi katika njiapanda, ikizingatiwa walikuwa wakiitegemea kujiendeleza kimaisha kutokana na  kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira nchini.

Mnamo Februari, Rais William Ruto alisema amekuwa akizungumza na  mashirika kadhaa ya kutoa ajira za mitandaoni, ili kuwafaidi vijjana nchini wasio na ajira.

Rais alisema kuwa miongoni mwa mashirikka hayo ni Remotasks.

“Nimezungumza na mashirika kadhaa ya  kutoa ajira za mitandaoni iili kuhakikisha yanawafaa maelfu ya vijana wasio na ajira  nchini. Kutokana na hayo, serikali itaanza mikakati ya kuweka mtandao wa intaneti kote nchini ili kuhakikisha kuwa vijana wamepata nafasi ya kufanya kazi hizo,” akasema Rais.

Kampuni hiyo ni miongoni mwa mashirika makubwa makubwa nchini Amerika ambayo yamekuwa yakitoa ajira za mitandaoni kwa mamilioni ya waatu kote duniani.