Maelfu watoroka makwao baada ya volkano kulipuka

Maelfu watoroka makwao baada ya volkano kulipuka

Na AFP

MAELFU ya watu walitoroka makwao baada ya volkano kulipuka na lava kusambaa kutoka Mlima Nyiragongo kufika jiji la Goma, DRC jana.

Hata kabla ya tangazo rasmi kutolewa kuhusu kutokea kwa mkasa huo, watu walionekana katika barabara za jiji hilo wakibeba mali yao kujitafutia maeneo salama.

Volkano hiyo, iliyoko umbali wa kilomita 10 (maili sita) kutoka Goma, ililipuka mara ya mwisho mnamo 2002 na kuua watu 250 huku watu wengine 120,000 wakipoteza makazi.

“Mbingu imegeuka nyekundu,” mkazi mmoja, Carine Mbala, aliambia AFP.

“Kuna harufu ya madini ya salfa kote. Kwa umbali unaweza kuona wingu la moto likitoka mlimani,” mama huyo akaeleza.

Mamlaka ilisema mtitiriko wa lava ulikuwa umefika katika uwanja wa ndege wa Goma, ulioko viungani mwa jiji hilo karibu na Ziwa Kivu. Hii ni licha ya wakazi kusema lava hiyo ilifika katika ua la uwanja huo wa ndege.

“Hali inaendelea kuwa mbaya,” afisa mmoja kutoka Mbuga ya Kitaifa ya Virunga, ambako volkano hiyo inapatikana, aliwaambia wafanyakazi wake kupitia taarifa.

Waziri wa Mawasiliano, Patrick Muyaya, alithibitisha Jumamosi kwamba serikali imeanza mpango wa kuwaokoa watu.

“Serikali inajadiliana kuhusu hatua za dharura itakayochukua.” akaeleza.

Wakati huo huo, Rais wa DRC Felix Tshisekedi Jumamosi alisema atakatiza ziara yake Uropa na kurejea nyumbani Jumapili kuendesha shughuli ya utoaji misaada kwa waathiriwa wa mkasa huo.? Mapema jana, angalau watu 3,000 walikuwa wamewasili taifa jirani la Rwanda kujisalimisha kutokana na athari za mlipuko huo wa volkano.

Shirika la Habari la Rwanda liliweka picha kwenye twitter za watu waliokuwa wakiwasili katika wilaya ya Rubavu, likiongeza kuwa watu hao watapewa hifadhi katika shule na maeneo ya maabadi.

Watu walioanza kuondoka mji wa Goma hata kabla ya taarifa rasmi kutolewa mwendo wa saa moja za jioni Jumamosi. Volkeno hiyo ililipuka na kurusha na kurusha moshi mweusi angani.

Afisa huyo wa Mbuga ya Virunga jana alisema huenda mtiririko huo wa lava ukafika katika ufuo wa Ziwa Kivu.

“Mlipuko huu wa Mlima Nyiragongo ni sawa na ule uliotokea 2002,” akasema huku akiwashauri wakazi wanaoishi katika maeneo ya uwanja wa ndege wa Goma kuhamia maeneo salama.

Hata hivyo, alitoa hakikisho kuwa mitaa mingine ya jiji hilo ni salama na kwamba hakuna uwezekano kwamba mtiririko huo wa lava utafika maeneo hayo.

Umeme ulikatizwa katika maeneo kadha ya jiji mamia ya watu walipoanza kuondoka makwao.

You can share this post!

Mswada wa mbunge kuinua sekta ya sukari

Pambano kali kushuhudiwa Kiambu Ruto akikabili Uhuru