Habari

Maeneobunge maskini kupata mgao mkubwa wa NG-CDF

September 19th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MAENEOBUNGE yenye viwango vya juu vya ugumu wa maisha yatapokea mgao mkubwa wa fedha za Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF) ikiwa mswada wa marekebisho ya sheria ya hazina hiyo itapitishwa.

Mswada huo ambao umedhaminiwa na Mbunge wa Tongaren Eseli Simiyu unapendekeza kigezo cha ugavi wa fedha hizo ubadilishwe ili asilimia 75 zigawanywe kwa usawa na asilimia 25 zisambazwe kwa misingi ya viwango vya umasikini katika kila eneobunge.

Kwa mujibu wa sheria ya sasa maeneo bunge yote 290 hupata mgao sawa wa fedha ambazo hutengwa kufadhili miradi ya maendelezo kila mwaka, bila kuzingatia mahitaji maalum ya kila sehemu.

Kwa mfano, katika mwaka huu wa kifedha Sh39.8 bilioni zimetengwa kwa hazina ya NG-CDF, ambapo ina maana kwamba kila eneobunge litapokea mgao sawa wa Sh137.5 milioni.

Lakini Bw Eseli, kupitia mswada anapendekeza katika mswada wake kwamba thuluthi tatu ya pesa hizi (takriban Sh29.8) zigawanywe kwa usawa huku robo (Sh10 bilioni) zigawanywe kwa misingi ya kiwango cha umasikini katika kila eneobunge.

“Mswada huu unaifanyia marekebisho sheria ya sasa ya hazina ya NG-CDF ili kuhakikisha kuwa maeneo bunge ambayo yameachwa nyuma kimaendeleo kwa misingi ya viwango vya umasikini yanaimarika,” sehemu ya mswada huo inasema.

Kulingana na mswada huu mfamo ufadhili wa miradi ya maendeleo katika maeneo bunge unapasa kuzingatia, inavyopendekezwa katika kikatiba ya sasa.

Mfumo wa sasa

Dkt Simiyu anasema kuwa mfumo wa sasa wa ugavi wa fedha za hazina ya NG-CDF unapendelea maeneobunge yaliyofikia viwango vya juu kimaendeleo ikilinganishwa na yale yaliyobaki nyuma “kutokana na sababu za kisiasa na kihistoria.”

“Maeneobunge kama yale yanayopatikana katika maeneo kame na yenye viwango vya juu vya umasikini yanapasa kutengewe kiwango cha juu cha fedha za hazina ya NG-CDF. Hatua hii itayawezesha kufikia viwango vya maeneobunge mengine yaliyopaa kimaendeleo kama yale yaliyo karibu na miji mikuu,” Dkt Eseli akaongeza.

Ikiwa mswada huu utapitishwa na kuwa sheria, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu hazina ya NG-CDF Moses Lessonet atalazimika kuchapisha mwongozo mpya wa mpya wa ugavi wa fedha hizo baini ya maeneo bunge 290.

Pesa za hazina hii hutumika kufadhili miradi ya elimu na usalama pekee, yaliyoko chini ya usimamizi wa serikali ya kitaifa.