Habari Mseto

Mafisadi, baadhi ya asasi zimeishika Kenya mateka – ripoti

August 2nd, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

MIAKA miwili iliyopita mwezi Agosti , wiki kama hii, uchaguzi mkuu ulikuwa swala kuu kwani ulikuwa karibu kufanyika.

Uchaguzi wa urais wa mwaka 2017 unasalia kuwa wa kihistoria kwani ndio wa kwanza nchini kutupiliwa mbali na mahakama ya juu zaidi.

Matukio ya mwaka 2017 yamenakiliwa katika ripoti ya kurasa 95 ambayo inazungumzia hali ya Kenya “kutekwa nyara na baadhi ya watu na asasi ” maarufu kama “deep state”.

Ripoti hiyo inajulikana kama ‘Exposing the Governance Conundrum in Kenya: Deep State, Mega Corruption and Stalled Electoral Reforms’.

Ripoti hiyo ambayo ilitolewa Jumanne na Tume ya Haki za Binadamu Nchini (KHRC), inaonyesha kile inataja ni uchaguzi huo kufanyika kwa njia isiyofaa kutokana na ushirikiano baina ya wanasiasa na vitengo mbalimbali serikalini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, mkurugenzi mkuu wa International Centre for Policy and Conflict Bw Ndung’u Wainaina alisema kuwa Tume ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) ni ya kulaumiwa kwa idadi kubwa ya viongozi mafisadi serikalini.

“IEBC iliwapa nafasi wanasiasa 106 ambao hawakufaa kuwa katika ofisi za serikali kwa sababu ya doa la ufisadi,” alisema Bw Wainaina.

Ripoti hiyo pia inaangazia ufisadi na madhara yake nchini; na jinsi vitengo mbalimbali vimechangia katika changamoto hiyo.

Kulingana na mkurugenzi wa Inuka Kenya John Githongo, kwa zaidi ya miaka 25, Kenya imepigana na ufisadi bila mafanikio.

Mkurugenzi wa shirika la Inuka Kenya Bw John Githongo wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Julai 30, 2019. Picha/ Magdalene Wanja