Michezo

Mafisi sasa hawalali wakiwania penzi la ‘Shakira’

August 20th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

IZABEL ambaye ni mkewe kiungo wa Chelsea, Mateo Kovacic, 24, amekiri kunyemelewa mitandaoni na wanaume ambao kwa mtazamo wake wana nia ya kuvuruga uhusiano wa kimapenzi ambao amekuwa nao na mumewe kwa zaidi ya miaka mitatu.

Kwa mujibu wa kichuna huyo mwenye umri wa miaka 24, kuna wanaume ambao wamekuwa wakililihemea pakubwa penzi lake kwa kurusha jumbe za kumtongoza mitandaoni tangu Kovacic abanduke Real Madrid na kutua Chelsea kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Kipusa huyo ni msomi wa masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Zagreb, Croatia. Ni mfanyabiashara maarufu nchini Uhispania, Uswisi na Croatia alikopagazwa jina ‘Shakira’ kutokana na kushabihiana kwake na mwanamuziki huyo mzawa wa Colombia ambaye kwa sasa ni mkewe beki wa Barcelona, Gerard Pique.

Akihojiwa na gazeti la The Sun, Izabel aliungama kwamba wengi wa wanaume wanaomvizia ni wachezaji na mashabiki wa Chelsea ambao walimfahamu tu mwanzoni mwa msimu huu.

Madai ya Izabel yanajiri miezi michache baada ya Rebekah Nicholson ambaye ni Jamie Vardy wa Leicester City kufichua kuwa imelazimu siku hizi kujifungia nyumbani na kupunguza ziara za mara kwa mara alizozizoea hapo awali kwa hofu ya kutongozwa.