Makala

Mafunzo muhimu kuhusu ufugaji wa kuku na ng'ombe

March 7th, 2018 4 min read

Na FAUSTINE NGILA

FEBRUARI 24, 2018, Akilimali ilijumuika na jarida la kilimo kwa lugha ya Kiingereza Seeds of Gold katika kituo cha utafiti cha Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo nchini (Kalro), kilomita moja kutoka mjini Kitale, kaunti ya Trans Nzoia.

Mamia ya wakulima kutoka kaunti za Nairobi, Nyeri, Nakuru, Kakamega, Uasin Gishu, Bungoma, Kisumu na Trans Nzoia walimiminika katika kituo hicho, kila mmoja akitazamia kuelimishwa kuhusu mbinu bora za kilimo na jinsi ya kukabiliana na visiki vya ufugaji na ukuzaji mimea.

Wataalamu wa kilimo, wavumbuzi, kampuni mbalimbali na wapenzi wa kilimo walihudhuria hafla hiyo inayoandaliwa baada ya kila miezi miwili, kwa lengo moja la kuimarisha kilimo nchini.

Kipindi cha maswali na majibu kilianza kuhusu ufugaji wa ndege wa nyumbani, ambapo zaidi ya wafugaji kumi waliuliza maswali mbalimbali ambayo yamekuwa kitendawili kwao kwa muda mrefu.

Mkulima mmoja wa kundi la wafugaji la Shamba la Wanyama kutoka kaunti ya Kakamega aliuliza sababu ya kuku wake wa kienyeji kutoangua asilimia 100 ya mayai wanayolalia, vifaranga kufa ovyoovyo na jinsi ya kutokomeza mazoea ya kuku kula mayai.

Katika jibu lake, mkurugenzi wa kituo cha Kalro cha Kakamega Dkt Luvodicus Okitoi alianza kwa kuwauliza wafugaji mbinu zao za kufuga kuku.

“Ni mayai mangapi kuku wa kawaida anaweza kutaga kabla ya kuyalalia?” aliwauliza. Wakulima walitoa idadi iliyo kati ya 15 na 25, na kukubaliana 18 kama idadi ya wastani.

“Kuku yeyote wa kienyeji anayetaga zaidi  mayai 20 hawezi kuyalalia na yaangue yote. Idadi ya wastani ni mayai 14 na idadi ya vifaranga watakaoanguliwa itakuwa 10 na watakaofikisha umri wa kukomaa ni sita,” wakulima walikubaliana na kauli hiyo.

Mtaalamu huyo alielezea kuwa bei ya kuku mmoja mjini Bungoma ni Sh500, na ikizingatiwa kuwa kuku hawa hutaga mayai mara tatu kwa mwaka, mkulima hupata Sh9,000 kwa mwaka.

Wafugaji wa kuku waliuliza kila aina ya maswali kwenye kliniki ya Seeds of Gold iliyofanyika katika kituo cha Kalro, Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila

Kuongeza mapato
Akielezea jinsi ya kuongeza kiwango hiki cha pesa kutoka kwa kuku mmoja, alisema, “Iwapo kuku atalishwa vizuri, vifo vitapungua. Badala ya kumpa kuku mayai 14, mpe mayai 10 na ataangua yote na vifaranga wote wafikie umri wa kukomaa.”

Mkulima mwingine aliuliza kuhusu kuku kufikia kikomo cha kutaga mayai.

“Unaweza kupyesha uwezo wa kuku kutaga mayai. Mtumbukize kuku ndani ya maji baridi. Baada ya hapo, homoni zake zitabadilika na kuanza kutaga mayai tena.

Kwa kufanya hivi, kuku wako anaweza kutaga mayai mara kumi kwa mwaka, ikilinganishwa na mara tatu bila mbinu hii,” akajibu.

Kwa hilo, wakulima waliduwazwa na mbinu hiyo, na baada ya kupiga hesabu za haraka, waligundua kuwa badala ya Sh9,000 wanazopata kila mwaka, wanaweza kuuza kuku kumi mara kumi kwa mwaka na kutia mfukoni Sh50,000.

Mfugaji auliza swali kwenye kliniki ya Seeds of Gold iliyofanyika katika kituo cha Kalro, Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila

Kuku mlezi
Ili kudumisha ubora wa ndege wanaofuga, wakulima walishauriwa kuvalia njuga ufugaji wa kuteua kuku mmoja ambaye atawalea vifaranga wote.

“Chagua kuku wako bora kwa kulea vifaranga na ataweza kukulelea vifaranga wote 100 walioangaliwa na kuku kumi tofauti,” akashauri mtaalamu huyo.

“Je, hili litawezekanaje?” akauliza mfugaji mmoja aliyeshangazwa na mbinu hiyo.

Daktari huyo alielezea kuwa ingawa kila kuku anajua vifaranga wake kwa harufu, vifaranga wa kuku wengine wanaweza kuletwa kwa kuku mlezi usiku kwa kutumia mikono safi.

Kufikia asubuhi, harufu hiyo itakuwa imeyeyuka na kuku mlezi atawakubali vifaranga wote. Akikataa, basi ujue ulikuwa na marashi kwa mikono yako.

Francis Mathai aonyesha nduma aina ya Dryland aliyopendekezewa na maafisa wa Kalro Mei 2017. Alikuwa amehudhuria kliniki ya mafunzo ya kilimo mjini Kitale Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila

Kugeuza kuku kuwa kiangulio
Mtafiti huyo pia alielezea wakulima jinsi ya kugeuza kuku wao kuwa mashine ya kuangua vifaranga. Aliwashauri kuteua kuku aliye na rekodi nzuri ya kuangua mayai yote.

“Mpe kuku huyo mayai 10 baada ya kila siku 21. Mpe mayai yaliyotagwa na kuku wengine alalie katika siku ya 22. Baada ya kila siku 21, vifaranga 10 walioanguliwa watakuwa na afya njema mpaka waishi mpaka ukomavu. Hivyo, kuku huyu anahitaji chakula na maji ya kutosha.”

Kwa mwaka mmoja, utaangua vifaranga mara 17 watakaolelewa na kuku walezi, na hivyo mfugaji atapata Sh85,000 akiwa mashinani.

Kuhusu utata wa ufugaji wa kuku wa umri tofauti na kuwatibu, Dkt Okoiti alianza kwa kuwakumbusha wafugaji kuwa yai la kwanza kutagwa haliwezi kuangua kuwa kifaranga.

“Pasua yai hilo na ujaze changarawe na ufunike ganda lake. Yai hili feki utaliweka kwa kiota baada ya kuchukua yai lililotagwa. Kuku hupata motisha wa kutaga akiona yai kiotani.”

Aliwataka wafugaji kutia alama mayai yote kuhusu siku yaliyotagwa. Baada ya kati ya siku7-10 tangu kutagwa, mayai yatakuwa tayari kulaliwa na kuangua vifaranga wa umri sawa.

Mkurugenzi wa kituo cha Kalro kaunti ya Kakamega Dkt Ludovicus Okitoi akiwaelimisha wafugaji wa kuku kuhusu mbinu mbalimbali za kuongerza mapato mjini Kitale Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila.

Kupunguza vifo
Ili kukomesha tatizo la vifaranga kufa, aliwashauri kufuga jogoo mmoja kwa kila kuku 10 ambaye hana ukoo na mamake ili kuimarisha uwezo wa mayai kuangua na kuepuka vifaranga kufa.

Kuku wanaokula mayai na kuwala wenzao manyoya, inamaanisha wamesongamana sana na mwangaza huwa mwingi katika kiota ambamo mayai hutagiwa.

Wakigundua ni tamu, hii sasa huwa tabia yao. Kwa hivyo, unafaa kuwakata midomo ukitumia kisu moto ili iwe butu, na watakomesha tabia hiyo kwa muda wa wiki mbili.

Wakiwachanja kuku dhidi ya ugonjwa wa Newcastle, wafugaji walishauriwa kufanya hivyo mwishoni mwa kiangazi au mwishoni mwa msimu wa mvua.

“Je, kuku anaweza kuishi kwa muda gani kwa maisha yake?” mtafiti huyo akatupiwa swali.

“Maisha ya kuku yanategemea mbinu za mfugaji,” alianza.

“Kama nyoka, kuku huondoa magamba yake. Ukiona manyonya yakimtoka, mlazimishe kutoa maganda. Manyoya mengi huashiria ukosefu wa maji na chakula. Mnyime maji na chakula kwa wiki nzima, hawezi kufa. Baada ya hapo atapyesha homoni za kukua na kuanza kutaga mayai upya. Hivyo ndivyo unaongeza maisha yake.”

Wakuzaji wa miche ya matunda, mitishamba na mboga waonyesha ubunifu wao. Picha/ Faustine Ngila

Chakula cha ng’ombe
Maswali sasa yaliegemea ufugaji wa ng’ombe. “Je, ni nafaka zipi bora zaidi kwa kutengeneza chakula cha ng’ombe?” akauliza mfugaji wa kike.

Mkurugenzi wa kituo cha Kalro, Kitale Dkt F Lusweti alijibu kuwa mtama na mahindi ni chaguo bora.

“Kalro inapendekeza mahindi aina ya KH5500-43A kwa kuwa inakomaa haraka na unaweza kukuza alizeti baada ya kuvuna.

Iwapo unataka chakula chenye proteini, basi tumia mahindi mbichi wakati yameanza kuunda maziwa.

Lakini kama unataka chakula kingi kisicho na proteini nyingi, tumia mahindi yakiwa kiwango cha kuchemshwa. Nyasi ya Rhodes pia ni nzuri.”

Swali liliibuka kuhusu nyamakondo (placenta) kukwama ndani ya baadhi ya ng’ombe baada ya kuzaa.

Mtaalamu huyu alisema sababu kuu ni ya kiukoo, jua kali au ndama kuwa mkubwa kupita kiasi. Aliwashauri wafugaji kusaka fahali wanaozalisha ng’ombe ndama wa wastani.

Kampuni ya Simba Corp iliwaelezea wakulima trakta na mashine bora za kilimo na ufugaji inazounda. Picha/ Faustine Ngila

‘Hongo kwa ng’ombe’
Watafiti walionya wafugaji dhidi ya ‘kuwahonga’ ng’ombe kabla ya kumkama, kwa kumlisha chakula cha ng’ombe wa maziwa. Walisisitiza kuwa inafaa ng’ombe watunukiwe kwa kumpa mfugaji maziwa, na si kinyume chake.

Wafugaji pia walionywa dhidi ya kufuga fahali ikiwa wana ng’ombe watano pekee. Gharama ya kumfuga iko juu, hivyo mkulima anafaa kutumia mbinu ya kiteknolojia kuwatunga mimba ng’ombe.

Chuo Kikuu cha Egerton kilitangaza kuwa kimevumbua aina mpya ya mtama inayoweza kutumika kwa uokaji wa mikate. Kilisema kinashirikiana na kampuni za uokaji ili kuitangaza sokoni.

Wote waliohudhuria darasa hilo la elimu ya kilimo walifurahia kupata ujuzi na mbinu mpya za kupunguza gharama, kukabiliana na magonjwa, kuongeza mavuno na kuepuka hasara katika kilimo chao.

 

Baruapepe: [email protected]