Habari za Kitaifa

Mafuriko bara yapeleka madhara Lamu kunakoshuhudiwa kiangazi

May 17th, 2024 4 min read

NA KALUME KAZUNGU

LICHA ya Lamu kuendelea kushuhudia kiangazi kila mara, inaathiriwa vibaya na mvua kubwa na mafuriko yanayoshuhudiwa katika maeneo mengine ya Kenya, hasa bara.

Hii ni kutokana na kwamba maji yanayomiminika kutoka nyanda hizo za juu yamekuwa yakishuhudiwa kutiririka hadi kufika Lamu kupitia Mto Tana.

Hali hiyo imekuwa ikiacha baadhi ya vijiji na hata barabara zikisombwa na mafuriko wakati kiangazi kikichapa eneo hilo.

Miongoni mwa vijiji ambavyo vimekuwa vikijipata katika dhiki ya mafuriko wakati ukame ukitafuna Lamu ni Chalaluma, Moa, Gamba na maeneo mengine yaliyo viunga vya tarafa ya Witu.

Kwa mfano, kijiji cha Chalaluma kwa sasa kimeshuhudia maji yakikizingira, hali ambayo imepelekea wakazi kushuhudia ugumu wa kuingia na kutoka kijiji hicho.

Wakati shule zilipofunguliwa kwa muhula wa pili juma hili, walimu wanaohudumia shule ya msingi ya Chalalula walilazimika kutumia ngalawa kuvuka na kuingia shuleni humo kufunza.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Mkurugenzi wa Elimu, Kaunti ya Lamu, Bw Zachary Mutuiri alikiri kuwa shule nyingi za eneo hilo hazikuwa zimeshuhudia mafuriko isipokuwa Chalaluma.

“Karibu asilimia 90 ya shule za Lamu zimefunguliwa. Hapa hatuna tatizo la mafuriko kwa shule zetu nyingi kama vile inavyoshuhudiwa bara. Ni shule ya Chalaluma pekee ambayo imezingirwa na maji. Walimu wangu wamelazimika kutumia mashua kuvuka kuingia shuleni kufunza,” akasema Bw Mutuiri.

Katika kipindi cha karibu majuma mawili sasa, mafuriko ya bara pia yameitumbukiza Lamu katika hali ya mkanganyiko na giza.

Hii ni baada ya mafuriko hayo kuisomba na kuikata barabara ya Lamu-Witu-Garsen, hasa eneo la Gamba.

Hali hiyo imetatiza usafiri kwani magari yanayohudumu kwenye barabara hiyo hayawezi kuvukisha abiria moja kwa moja hadi sehemu wanakohitajika.

Hapa, abiria wamelazimika kutumia ngalawa, mashua na boti kuvuka sehemu hiyo ya Gamba, iwe ni ikiwa wanaelekea Mombasa kutoka Lamu au kutoka Lamu kuelekea Mombasa.

Hali hiyo pia imeongeza gharama ya usafiri kwani abiria hulazimika kutoa fedha za ziada ili kuvukishwa na ngalawa, boti au mashua eneo hilo la Gamba, nauli ikiwa ni kati ya Sh300 na Sh400.

Isitoshe, maduka ya Lamu yaamekuwa yakikosa shehena zinazofaa za bidhaa kwani malori ya kusafirishia bidhaa hizo hayawezi kuvuka kuingia Lamu.

Ikumbukwe kuwa bidhaa nyingi za kibiashara, ikiwemo vyakula vinavyouzwa maduka ya Lamu hutoka nje ya kaunti hiyo, hasa Malindi na Mombasa.

Kutokana na mafuriko ya bara yaliyoikata barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen, baadhi ya wanabiashara wamelazimika kusafirisha bidhaa zao kupitia njia ya boti kutoka Ngomeni au Malindi kaunti ya Kilifi na hata Mombasa kuviingiza kisiwa cha Lamu kupitia usafiri wa mashua baharini.

Bw Abdalla Ali, mmoja wa wanabiashara wa maduka ya jumla kisiwani Lamu, anasema usafirishaji bidhaa kutoka mbali, hasa Malindi, Ngomeni na Mombasa kuingia kisiwa cha Lamu kwa kutumia boti ni ghali mno.

Bw Ali anasema wanafanya jitihada zote hizo ili kuzuia Lamu kukumbwa na uhaba wa vyakula na mahitaji mengine ya kibinadamu.

“Kusafirisha shehena nzima ya bidhaa za kibiashara kutumia mashua baharini kutoka sehemu kama vile Malindi au Mombasa hadi Lamu si chini ya Sh100,000. Kukatizwa kwa barabara yetu na mafuriko kumeitumbukiza Lamu katika hali ya dhiki. Twajikaza kama wanabiashara ili wakazi hapa wasikumbwe na ugumu wa maisha na uhitaji wa kibinadamu wakishuhudia uhaba wa bidhaa madukani,” akasema Bw Ali.

Dhiki nyingine inayochangiwa na mafuriko ya bara yaliyoiacha barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen kukatika ni kukwama kwa usafirishaji mizigo kupitia malori au trela kutoa bandari ya Lamu kuelekea maeneo mengine ya nchi na mataifa jirani.

Bandari ya Lamu inapatikana eneo la Kililana, Lamu Magharibi.

 Tegemeo kubwa la kubeba na kusafirisha mizigo inayofikishwa bandarini humo kwa meli kuelekea sehemu zingine za nchi na mataifa jirani ni barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen ambayo kwa sasa imekatwa eneo la Gamba.

Malori yanayotoka maeneo kama vile Nairobi na sehemu zingine hayajaweza kufika au kutoka bandarini Lamu kwani hakuna barabara ya kupitia.

Kwa mfano, Jumamosi wiki iliyopita, bandari ya Lamu ilipokea shehena kubwa zaidi ya mbolea kutoka nchini Morocco.

Mbolea hiyo ya tani 60,000 ilifikishwa bandarini Lamu kupitia meli ya Ethiopia kwa jina Abbay II.

Mbolea hiyo ilihitajika kufikishwa nchini Ethiopia kupitia usafiri wa barabarani ambao ni wa malori na trela.

Hali ya mafuriko ilivyo kwa sasa Gamba imezuia shehena hiyo ya mbolea kusafirishwa hadi ilikohitajika, hivyo kuchelewa kwa kipindi cha karibu juma nzima sasa.

Barabara iliyokarabatiwa eneo la Gamba katika Kaunti ya Lamu. PICHA | MAKTABA

Wakati wa ziara ya kutathmini miundomsingi ya Mradi wa Uchukuzi wa Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini (Lapsset) na ile ya barabara zilizoharibiwa na mafuriko juma hili, Waziri wa Barabara na Uchukuzi, Bw Kipchumba Murkomen alisema usafirishaji wa mbolea hiyo ya Ethiopia unahitaji angalau malori 2,400, hali ambayo itatoa ajira kwa wananchi wengi.

Bw Murkomen aliweka wazi kuwa Wizara yake iko mbioni kuona kwamba shehena hiyo ya mbolea iliyokwama bandarini Lamu inasafirishwa haraka iwezekanavyo.

Alisema huku wakisubiri mafuriko kupungua eneo la Gamba kupisha ukarabati wa barabara ya Lamu-Witu-Garsen kutekelezwa, pia yuko mbioni kuharakisha ujenzi na kukamilika kwa mradi wa barabara nyingine ya umbali wa kilomita 256 ya Lamu-Ijara-Garissa.

Alisema matarajio yake ni kuona barabara hiyo ya Lamu-Ijara-Garissa ikikamilika kufikia Februari 2025, akiitaja kuwa yenye natija kwani itasaidia pakubwa usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini Lamu.

“Bandari ya Lamu ni kiungo muhimu katika kuboresha uchumi wa taifa hili. Wakati barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen ikiwa imekatwa na mafuriko, na tunaposubiri ujenzi baada ya maji kupungua, bado nitaendelea kusukuma. Twataka kuona kwamba shehena ya mbolea inayolenga kufikishwa Ethiopia kutoka bandarini Lamu inasafirishwa haraka iwezekanavyo,” akasema Bw Murkomen.

Wakati wa ziara ya Lamu, Bw Murkomen alifichua kuwa kati ya Sh26 bilioni na Sh30 bilioni zinahitajika kukarabati na kujenga miundomsingi, ikiwemo barabara na vivuko vilivyoharibiwa na mafuriko yanayoshuhudiwa kote nchini.

Mafuriko ya Lamu inayoshuhudia ukame mara nyingi huchangiwa zaidi na Mto Tana kuvunja kingo zake, hasa baada ya maji ya mabwawa kama vile Seven Folks yaliyoko bara yanapojaa kupita kiasi hadi kumwagika.