Habari za Kitaifa

Mafuriko: Daraja la Oldonyo Sabuk halipitiki

May 4th, 2024 2 min read

NA LAWRENCE ONGARO

SERIKALI imeombwa kukarabati daraja la Oldonyo Sabuk katika eneo la Kilimambogo, Thika Mashariki lililoharibiwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa inayonyesha maeneo mengi nchini.

Daraja hilo huunganisha kaunti za Kiambu na Machakos.

Mbunge wa Thika Bi Alice Ng’ang’a mnamo Ijumaa alizuru eneo hilo na kujionea mwenyewe jinsi daraja hilo lilivyobomoka na kukatiza shughuli zote za uchukuzi kati ya kaunti ya kaunti hizo mbili katika eneo hilo.

Bi Ng’ang’a alitoa wito kwa wakazi wa maeneo hayo wawe makini zaidi wanapokaribia sehemu hizo kwa sababu uzito wa maji ni mkubwa ajabu.

“Tunaelewa mvua ya masika bado inaendelea na kwa hivyo, kila mmoja wetu ni lazima awe makini asisombwe na maji yanayotamba kwa kasi,” alisema mbunge huyo.

Alisema mvua imeathiri shughuli za biashara ambapo hata hakuna usafiri ambao unafanyika katika eneo hilo kwa zaidi ya wiki mbili sasa.

Mbunge wa Thika Bi Alice Ng’ang’a akiwa eneo la Kilimambogo. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Sekta za matatu na bodaboda zimeathiriki huku wakazi wa pande zote mbili wakiwa hawana mbinu yoyote ya kuvuka daraja hilo.

Ni kubaya ajabu.

Mbunge huyo alitoa wito kwa serikali ya kaunti ya Kiambu kufanya hima kuona ya kwamba inarekebisha mabomba ya majitaka ili yasije yakachanganyikana na uchafu uliosombwa na maji ya Mto Athi uliovunja kingo zake.

Anahofia maradhi ya kipindupindu yanaweza kulipuka kutokana na hali ilivyo kwa hivyo alitoa wito watu wachemshe maji ya kunywa kila mara.

Mwakilishi wadi wa Ngoliba Joachim Mwangi alipendekeza serikali kuu itoe tingatinga la jeshi ili kuchimba mitaro ya kupisha maji mengi yanayoenea kila mahali.

“Wakazi wa eneo langu la Ngoliba wamepata pigo kubwa kwa sababu mafuriko yamevamia makazi huku mashamba yao yakifunikwa na maji,” alifafanua Bw Mwangi.

Alitoa wito serikali ifanye hima kuingilia kati janga linalokumba wakazi wa Kilimambogo na wale wa Machakos litatuliwe.

Mhudumu wa bodaboda, Bw Joseph Musyoki wa Oldonyo Sabuk alisema biashara yake imekwama kwa zaidi ya wiki mbili sasa.

“Mimi tangu daraja libomoke sijaendesha pikipiki yangu kuvuka ng’ambo ya pili kuelekea Machakos kutokana na mafuriko,” akasema Bw Musyoki.

Alisema hata boti zilizokuwa zikivusha wakazi wa eneo hilo zimekwama kutokana na maji kufurika na kukimbia kwa kasi.