Habari za Kitaifa

Mafuriko: Viongozi wa kidini wawarai Wakenya kumrejelea Mungu

May 2nd, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

VIONGOZI wa kidini, sasa wanawarai Wakenya na ulimwengu kumrejelea Mungu ili kujiokoa kutokana na majanga mbalimbali, yakiwemo mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa.

Katika mahojiano na Taifa Leo, viongozi hao, wakiwemo maimamu, masheikh, mapadri na makasisi walieleza kusikitishwa kwao na jinsi ambavyo watu, wengi wakiwa ni watoto na wanawake, wamekuwa wakiangamia kila kuchao kutokana na mafuriko.

Kwa kumrejelea Mungu na kutubu, viongozi hao wanasema Mungu ataondoa majanga mbalimbali yanayoandama taifa la Kenya, yakiwemo mafuriko. Wanadai kukithiri kwa ufisadi, dhuluma za kila aina, mauaji, ndoa za jinsia moja ulimwenguni miongoni mwa masuala mengine kuwa ni mambo yanayomchukiza Mola ambayo nchi na ulimwengu wafaa kutubu

Jumatano, miili miwili iliopolewa katika mto wa msimu kufuatia mafuriko Kitengela, Kaunti ya Kajiado huku idadi ya waliopoteza maisha eneo la Mai Mahiu, Kaunti ya Nakuru ikipanda hadi 52.

Aidha tangu mafuriko kuanza nchini takriban watu zaidi ya 170 wameuawa ilhali karibu 200,000 wameachwa bila makao.

Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu Kenya (CIPK), tawi la Lamu, Abubakar Shekuwe, alishikilia kuwa vile ambavyo Waislamu hulazimika kufanya dua maalum wakati kunaposhuhudiwa ukame nchini kumuomba Mungu alete mvua, vilevile kunayo maombi ya kumsihi Mwenyezi Mungu kuondoa balaa za mvua na badala yake kuleta mvua ya wastani, yenye matunda na manufaa.

“Tunavyofahamu ni kwamba ghadhabu ya Mungu huwa athari zake ni kubwa na zenye kishindo. Sisemi kwamba yanayotendeka nchini ni adhabu ya Mungu. La hasha. Ila huu ni wakati wetu waumini wote kumsongelea karibu zaidi Mwenyezi Mungu. Tumuombeni ili badala ya mvua tunayoshuhudia kuwa ya maafa, aigeuze ili iwe ya baraka na matunda kwetu,” akasema Bw Shekuwe.

Kauli yake iliungwa mkono na Ustadh Mahmoud Ahmed Abdulkadir, maarufu kama Mau.

Lakini Bw Mau alitaja baadhi ya mambo yanayofanyika nchini na ulimwenguni kuwa yasiyomridhisha Allah (Mungu).

Aligusia mambo kama ufisadi, dhuluma, iwe ni ya ndani ya serikali au wananchi wenyewe kwa wenyewe, uabudu wa shetani, ndoa za jinsia moja, mauaji, na maovu mengineyo mengi kuwa masuala yanayomuudhi Mungu.

Alishikilia haja ya waumini wa dini zote kutubu na kumnyenyekea Mwenyezi Mungu ili kuiokoa Kenya na ulimwengu kutokana na majanga mbalimbali.

“Katika ulimwengu wa sasa, binadamu amegeuka kuwa mkaidi. Watu hawataki kumheshimu au kumuogopa Mola wao. Na ndiyo sababu utawapata wakiidhinisha ndoa za jinsi moja na mambo mengine mengi ambayo ni kinyume kabisa na yale Mungu anaruhusu. Ndiyo sababu tunasisitiza kwamba tujishushe na kumkaribia huyu Mungu ili ghadhabu yake kwa mwanadamu ipungue,” akasema Bw Mau.

Kauli za viongozi hao wa Kiislamu pia ziliungwa mkono na viongozi wa Kikristo.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis alisema Jumatano kuwa ameguswa na Wakenya kipindi hiki wakikabiliana na mafuriko ya maafa.

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa X (zamani Twitter), kiongozi huyo wa kidini alitoa wito wa maombi maalum kwa waathiriwa wa janga hili la kiasili.

“Ninafuatilia kwa karibu yanayojiri nchini Kenya kipindi hiki raia wakikabiliana na mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya watu wengi na kuharibu maeneo mengi. Tuombe sote kwa ajili ya wale ambao wanatatizika kufuatia janga hili la kiasili,” aliandika Papa Francis.

Askofu Jeremiah Kikuvi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Muungano wa Lamu Pastors Fellowship, alisisitiza suala la watu kumgeukia Mungu, kutubu na kunyenyekea, akiamini kuwa kufanya hivyo kutaiponya nchi ya Kenya na ulimwengu kutokana na majanga.