Habari za Kaunti

Mafuriko: Waliotafuta hifadhi shuleni waingiwa na wasiwasi

April 25th, 2024 2 min read

NA GEORGE ODIWUOR

WASIWASI mwingi unazikumba familia zilizohama makwao kutokana na mafuriko na ambazo kwa sasa zinakita kambi katika shule katika Kaunti ya Homa Bay huku likizo ya Aprili ikikaribia kumalizika wiki ijayo na shule nazo zikifunguliwa.

Familia zilizoha katika eneo la Rachuonyo Kaskazini zinaishi ndani ya madarasa ambayo yatatumiwa na wanafunzi wakati muhula wa pili utakapoanza.

Ilani tayari imetolewa kwao kutafuta makazi mahali pengine, ikiwezekana katika makanisa na maeneo mengine ya kijamii ili kuwapa wanafunzi nafasi na muda wa kutosha wa kusoma.

Shule za msingi za Osodo na Kobala katika kata ya Wang’Chieng’ ndizo zilizoathirika zaidi huku familia nyingi zilizohamishwa zikigeuza taasisi za masomo kuwa makazi ya muda.

Katika Shule ya Msingi ya Osodo, mwalimu mkuu, Walter Owino, alisema hali ya sasa huenda ikatatiza masomo shuleni.

Alisema taasisi hiyo ina idadi ya wanafunzi 750 kuanzia chekechea hadi Sekondari Msingi, baadhi yao kwa sasa wakiishi madarasani pamoja na wazazi wao.

“Takriban watu 400 wamekuja kutafuta makao shuleni. Wengi wa watoto hawadurusu sababu wengine wamepoteza vitabu vyao,” Bw Owino alisema.

Kulingana na mwalimu mkuu, familia hizo zitalazimika kuhama masomo yatakaporejea Jumatatu wiki ijayo.

Bw Owino aliiomba serikali na mashirika ya kutoa ya kibinadamu kibinadamu kuzipa familia zilizoathiriwa mahema ambayo wanaweza kutumia kama makazi ya muda.

Uongozi wa shule pia uliiomba serikali kuanzisha mpango wa lishe shuleni ili wanafunzi wabakie kuwa shuleni.

Familia nyingi katika eneo hilo zililalamika kwamba mafuriko yameharibu mazao yao mashambani na madukani.

Msaidizi wa Chifu wa Lokesheni Ndogo ya Kobala, Bw George Oburu alisema familia zilizoathiriwa zimekuwa shuleni kwa wiki mbili.

Alisema kuna uwezekano kwamba familia hizo zitaendelea kukaa madarasani katika wiki zijazo kwa sababu Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Nchini ilisema kwamba mvua itazidi kunyesha hadi mwezi Mei mwaka huu.

Kadhalika, Bw Oburu alisema takriban familia 580 kutoka eneo la Kobala zilhama makwao.

“Tunaomba serikali ya kitaifa na ya kaunti pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kusaidia familia zilizoathiriwa,” alisema.