Habari za Kaunti

Mafuriko yaamsha wanakijiji usingizini, yafagia mali

April 26th, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

BI Lona Andiema, mama wa watoto wanne katika kijiji cha Kambi Karai kilichoko katika wadi ya Sekerr, Kaunti ya Pokot Magharibi aliamshwa uzingizini ghafla na maji ya mafuriko usiku wa manane.

Maji hayo yalikuwa yameingia ndani ya nyumba yake.

“Kila kitu ndani ya nyumba kimeloa maji. Nguo zangu zote, chakula, bidhaa na vifaa vyote kwa nyumba vimeharibika. Watoto wangu wana hofu na hawana chochote cha kula,” akaeleza Bi Andiema alipotembelewa na Taifa Leo mnamo Ijumaa asubuhi.

Mkazi mwingine, Alex Musto alisema kuwa wakazi waliingiwa na hofu baada ya maji kuingia kwenye nyumba zao na kuharibu kila kitu.

“Watu walianza kupiga nduru wakitaka usaidizi huku kiwango cha maji kikiendelea kuongezeka. Wengi hapa kwa sasa hatuna makazi. Nyumba yangu imejaa maji,” akasema Bw Musto.

Alisema kuwa usiku wa mvua kubwa yeye pamoja na mkewe pamoja na wanawe watano walijaribu kuondoka kwenye nyumba lakini sakafu ilikuwa imejaa maji na wakashindwa kutoroka.

“Ilibidi tulale ndani ya maji. Tumepoteza mali na vifaa vyote vya nyumba na hata chakula,” akasema.

Hali ilivyo baada ya mafuriko katika kijiji cha Kambi Karai kilichoko katika wadi ya Sekerr, Kaunti ya Pokot Magharibi katika hii picha ya Aprili 26, 2024. PICHA | OSCAR KAKAI

Naye Simon Shau ambaye ni mfanyabiashara mwenye duka katika soko la Kambi Karai anasema kuwa bidhaa zake zote ziliharibiwa na maji.

“Nilipigwa na butwaa nilipofungua duka asubuhi kwa sababu kila kitu kilikuwa kimeharibiwa na maji hayo. Kijiji chote kimekuwa kama ziwa kubwa kufuatia mafuriko,” akasema Bw Shau.

Muuzaji huyo ambaye amebaki hohehahe alisema hajui ataanzia wapi tena baada ya kupata hasara.

“Mungu kuwa na huruma kwetu,” akasema.

Alisema kuwa eneo hilo ni hatari kutokana na ujangili na sasa wako kwenye hatari kubwa ya mashambulio.

“Tuku na hofu kwa sababu tunaweza kushambuliwa wakati wowote,” akasema.

Mafuriko hayo kutokana na mvua kubwa yalifagia viijiji katika eneo hilo na kuharibu makazi na kuacha eneo hilo bila chochote.

Hali ilivyo baada ya mafuriko katika kijiji cha Kambi Karai kilichoko katika wadi ya Sekerr, Kaunti ya Pokot Magharibi katika hii picha ya Aprili 26, 2024. PICHA | OSCAR KAKAI

Wakazi hao kwenye eneo hilo ambalo liko kwenye barabara kuu ya Kitale-Lodwar pia walipoteza mimea ya mazao ambayo ilisombwa na maji.

Mbali na Kambi Karai pia eneo la Porkoi katika lokesheni ya Sarmach liliathirika na mafuriko hayo.

Kulingana na wakazi hii inatokana na kukosekana kwa mfumo wa kupitisha maji katika eneo hilo.

Waathiriwa wanakadiria hasara kubwa ya mamilioni ya pesa baada ya mali zao kuharibika.

Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu, zaidi ya watu 600 wamepoteza makazi. Mnamo Alhamisi, kikosi cha kupambana na majanga cha shirika hilo kilizuru eneo hilo na kutathmini hali.

Zaidi ya maboma 93 yameathirika.

Kikosi hicho kilipeana ushauri nasaha kwa waathiriwa.

Mratibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika Kaunti ya Pokot Magharibi Scholastica Kapello ametoa wito kwa wakazi wawe wakizima stima wakati mvua inanyesha ili kuzuia maafa zaidi.

Alitoa wito kwa serikali kusambaza chakula, dawa na makazi kwa familia ambazo zimeathirika.

“Familia ambazo zimeathirika zinahitaji chakula, maji na fedha ili ziweze kujikimu na hata kuanza biashara ndogondogo,” akasema Bi Kapello.

Bi Kapello alitoa wito kwa wakazi kuhama eneo hilo kuenda maeneo salama zaidi.

“Tumewambia wahamie katika maeneo salama, eneo mojawapo likiwa ni shule ya Kambi Karai,” akasema.

Alisema kuwa itachukua muda kwa familia ambazo zimeathirika kurudi penye zilikuwa kutokana na janga hilo.

Afisa mkuu wa katika idara ya majanga katika kaunti ya Pokot Magharibi David Chepelion alisema kuwa wako na mipango ya kupeleka blanketi na magodoro kwa waathiriwa.

[email protected]