Makala

Mafuriko yalivyowaletea wakulima wa mahindi hasara

June 24th, 2020 3 min read

Na JOHN NJOROGE

[email protected]

Huku akionekana akiwa na wasiwasi lakini mwenye tumaini, Gerishon Kamotho anatazama ekari moja ya shamba lake ambalo liko eneo lililo sawasawa karibu na mtambo wa reli ambao hautumiki katika mji wa Elburgon katika kaunti ya Nakuru.

Akivalia shati ya rangi tofauti, suruali ndefu ya kijivu, kofia iliyofifisha na viatu nyeusi, Kamotho anajaribu kufukua mbaki za mimea ya mahindi zilizosalia baada ya mvua ya mafuriko kubemba mimea yake wiki chache baada ya kuzipanda huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha katika eneo hilo.

Mkulima huyu alisema kuwa alitumia zaidi ya shilingi elfu thelathini (30, 0000) wakati wa upanzi kwa kutayarisha shamba na kununua mbegu na mbolea.

“Mimea ya mahindi ilikuwa imemea na kunawiri vizuri ambapo baada ya wiki chache baada ya kumea, nilizinyunyizia dawa ya magugu na wadudu wanaovamia mimea huku nikitumia fedha zaidi,’’ akasema bwana Kamotho.

Alisema kwa wakati huo, mvua ilikuwa ya kadri na hakuna mtu yeyote angedhani kuwa italeta madhara makubwa shambani.

Wakati Akili Mali ilipotembea kwa shamba lake na mengineyo yaliyoadhiriwa na mafuriko hivi majuzi, Kamotho alikuwa akiwaza ni lipi ambalo angelifanya baada ya mimea kuharibiwa na mafuriko.

Alisema kuwa muda ulikuwa umeenda kwa kasi na nafasi ya kupanda mbegu zingine za mahindi ulikuwa duni.

“Msimu wa kupanda hasa kwa mahindi na vyakula zingine zinazokua kwa mwaka mmoja hulingana na muda fulani. Kwa wakati huu, muda wa kupanda hasa mahindi umepita na haziwezi kunawiri vizuri msimu unapoisha,’’ akasema Kamotho.

Mkulima huyu alikiri kuwa alitarajia kuvuna magunia yasiyopungua arobaini katika mwisho wa mwaka ambapo angepata zaidi ya shilingi elfu mia moja na ishirini (120,000).

Kamotho akiongea na Akili Mali alisema kuwa mimea iliyobaki ya mahindi ikinawiri, haiwezi tosha kulipia hata idadi ya pesa alizotumia wakati alipokuwa akinunua mbegu na mbolea.

Aliongeza kuwa ingawaje serikali ya kaunti ya Nakuru hutenga fedha za usimamizi zinazotumika nyakati za janga, hakuna yeyote kutoka idara hiyo aliyemtembelea kwa usaidizi.

“Hatujawaona wanaohusika na idara hiyo ya janga kutoka serikali ya kaunti. Tungewaomba maafisa hao watutembelee na kutusaidie ili tupate kufufua hasara iliyotupata,’’ akasema huku akiongeza kuwa kama walipa ushuru, serikali ina haki ya kuwapa msaada kutokana na janga hilo kama sehemu zinginezo.

Bwana Kamotho alisema kuwa wakulima wengi huwa na matumaini iwapo janga kama hilo hutokea ndani ya mashamba yao. Alikumbuka kuwa, kwa miaka miwili iliyopita alipata hasara ingine ya viazi alizozipanda katika ekari moja ya shamba.

“Nilikuwa nimepanda mbegu za viazi zilikuwa zimeidhinishwa na huduma ya ukaguzi wa mimea nchini (Kephis) katika ekari moja ya shamba. Kabla kuzivuna, ziliharibiwa na mvua ya mawe iliyokuwa ikinyesha wakati huo,’’ akasema.

Alipata hasara kubwa ambapo hata mbegu za kupanda kwa msimu mwingine hakupata.

Kwa wakati huo, gunia moja ya viazi ilikuwa inauza kwa shilingi elfu mbili (2,000) ambapo alitarajia kuvuna zaidi ya magunia arobaini kutoka kwa sehemu hiyo.

Hatua chache kutoka kwa bwana Kamotho, tunampata mkulima mwingine, Mwangi Kabiru ambaye mimea yake ya mahindi iliharibiwa na maji hayo ya mafuriko.

Huku akishikilia fimbo ndefu mkononi, Kabiru alikuwa pia anajaribu kutoa matawi ya mahindi yaliyofunikwa na matope katika shamba lake la ekari moja alilolipanda mahindi.

“Shamba langu ni la ekari nne lakini nafasi ya ekari moja iliyoharibiwa ni duni kufufuka lakini wakulima wenzangu wanatumamaini na vyakula hivyo iwapo mvua itapungua,’’ akasema Kabiru.

Siku mbili kabla ya mvua ya mafurika kunyesha, Kabiru alisema kuwa alinyunyizia mimea yake dawa ya kuua wadudu na magugu shambani. Dawa hiyo ilioshwa na maji ya mvua na kuacha uharibifu mkubwa shambani mwake na kwa majirani wenzake.

“Nilitumia zaidi ya laki moja na ishirini (120,000) kwa kutayarisha shamba, kununua mbegu na mbolea, kunyunyizia dawa na kazi yote iliyofanyika kwa ekari hizo nne. Katika ekari moja iliyoharibiwa, nilipata hasara zaidi ya shilingi elfu thelathini,’’ akasema bwana Kabiru.

Wakulima wengi wamepata hasara kubwa tangu mvua kubwa ilipoanza kunyesha wiki chache zilizopita.

Licha ya hasara kubwa waliyokubana nayo, wakulima wengi katika eneo hilo hawajachukua hatua ingine yoyote ya kuzuia janga kama hilo linapotokea wakati mwingine.

Bi Jane Wanjiru, alisema yeye hutembea mara kwa mara katika maonyesho ya kilimo na semina zinazo husiana na kilimo ambapo wakulima hupata maarifa na ujuzi mwingi.

“ Shamba langu liko mahali ambapo sio sawa lakini nimepanda nyasi kwa mpangilio ili kuzuia mmomonyoko wa udongo mvua kubwa inaponyesha,’’ akasema Muthoni.

Mkulima huyu alisema kuwa ametengeneza matuta na mitaro ili kuzuia mchanga wakati mvua kama hiyo ya mafuriko inaponyesha.

Afisa mmoja wa ukulima ambaye aliomba jina lake tulibane alisema wakulima huhimizwa kupanda miti ama matunda shambani mwao ili kuzuia mafuriko kama hayo yanayo haribu mimea yao.

“Pandeni miche ya avocado katika mashamba yenu na mafuriko kama hayo hayataadhiri mimea yenu,’’ akasema.

Mimea kama vile maharagwe na mbaazi ambayo huvunwa mwezi wa Agosti katika sehemu hii zilibebwa na maji na kuwaacha wakulima kwa hali ya kuchanganyikiwa na kuwaza mahali ambapo watazitoa mbegu zingine ifikapo msimu wa kupanda mwaka ujao.