Mafuriko yashuhudiwa mjini Thika

Mafuriko yashuhudiwa mjini Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Kisii mjini Thika wanaiomba serikali kufanya juhudi kurekebisha mabomba ya majitaka wakati huu mvua inapoendelea kunyesha.

Wakazi hao wanadai kuwa kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini wakazi wengi wameshuhudia maji yakifurika katika nyumba zao.

Bi Rose Wangithi aliye mkazi wa kijiji hicho anasema kuwa kwa siku chache zilizopita, wakazi wa eneo hilo wamepitia masaibu mengi huku maji yakifurika hadi katika nyumba zao.

Maji ya mafuriko katika kijiji cha Kisii mjini Thika. PICHA | MAKTABA

Kwa wiki moja iliyopita, wakazi wengi wamekuwa wakichota maji kutoka kwenye vyumba na kumwaga nje.

“Sisi kama wakazi wa eneo hili hatupati usingizi kwani tumebaki kuyaondoa maji yanayofurika hadi kwenye nyumba zetu,” alifafanua Bi Wangithi.

Anaeleza hata malandilodi wanaendelea kuhesabu hasara kwa sababu wapangaji wengi wameanza kuhamia maeneo mengine yasiyo na mafuriko.

Wakazi hao wanazidi kueleza ya kwamba hata biashara zimeharibika kutokana na kuyumba kwa usafiri wa magari.

“Barabara nyingi hazipitiki hivyo usafirishaji wa vyakula na bidhaa nyingine muhimu ni shida. Kwa hivyo, tunaomba usaidizi wa dharura,” alisema mkazi huyo.

Wanatoa wito kwa serikali ya Kaunti ya Kiambu na serikali kuu kufanya juhudi kuona ya kwamba hatua ya haraka inachukuliwa ili wakazi hao waendelee na shughuli zao za kawaida.

Walisema hata wanafunzi wengi wanapata shida ya kwenda shuleni kutokana na mafuriko hayo.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru achoshwa na hotuba yake mwenyewe

Watu 7.1 milioni wamepata chanjo dhidi ya corona kufikia...

T L