Habari Mseto

Mafuriko yatarajiwa tena Aprili

April 3rd, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MAFURIKO mijini na maporomoko ya ardhi katika nyanda za juu za nchi zinatarajiwa wakati msimu wa mvua ya masika unapoanza mwezi huu, idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini imesema.

Mkurugenzi wa idara hiyo, Bw Peter Ambenje, alitoa wito kuwe na maandalizi ya mapema kutoka kwa idara husika za serikali ili kuzuia hasara zinazoweza kusababishwa na hali hii ya hewa.

“Kuna uwezekano mkubwa miporomoko ya ardhi kutokea katika nyanda za juu za eneo la kati ikiwemo Murang’a na Meru, pamoja na Magharibi na Rift Valley. Hivyo basi inafaa mikakati iekwe kuzuia maafa na uharibifu wa mali,” akasema Bw Ambenje, kwenye taarifa.

Mvua kubwa imetabiriwa kunyesha maeneo ya Magharibi, Kaskazini Magharibi, Kati na sehemu kadhaa Kusini Mashariki.

Hata hivyo kutakuwa na uhaba wa mvua maeneo ya Pwani na sehemu kadhaa Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

“Mafuriko ambayo yanatarajiwa katika maeneo mbalimbali nchini yatatoa mandhari bora kwa ongezeko la mbu. Hii inatarajiwa kusababisha mkurupuko wa malaria. Hivyo basi Wizara ya Afya ya Umma inahimizwa kutambua maeneo ambapo mkurupuko unaweza kutokea na izidi kuchunguza magonjwa haya,” akasema Bw Ambenje.

Licha ya hayo, wakulima katika maeneo yanayotegemewa zaidi kwa uzalishaji wa chakula wamehimizwa kutumia msimu huu vyema ili wapate mazao bora.

“Inatarajiwa mimea itakua vyema katika maeneo mengi yanayotegemea kilimo kwa sababu mvua ya kutosha inatarajiwa kunyesha katika maeneo hayo. Kwa hivyo wakulima watumie vyema msimu huu wa mvua na watumie mbinu bora za kilimo ili wapate mavuno mengi zaidi,” akasema Bw Ambenje.

Vile vile, matokeo mengine mema yanayotarajiwa wakati wa mvua ya masika ni ongezeko la lishe ya mifugo katika maeneo ya wafugaji na ongezeko la maji katika mabwawa yanayutumiwa kuzalisha umeme.

Msimu huu unaanza baada ya mvua kubwa kushuhudiwa katika sehemu nyingi za nchi mwezi wa Machi ambapo kulitokea mafuriko yaliyosababisha maafa na uharibifu wa mali, mbali na kubomoka kwa barabara ya Mai Mahiu kuelekea Narok.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa ilisema mvua iliyonyesha machi ilikuwa ya kiwango kikubwa kuliko kawaida hasa katika maeneo ya Magharibi, Kati ikiwemo Nairobi, Kusini Mashariki na Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Kiwango cha juu zaidi kilikuwa Kakamega, Kericho, Kisii, Meru na Mtwapa huku kiwango cha chini zaidi kikiwa Lodwar, Garissa, Wajir, Mandera, Makindu na Voi.