Habari

Mafuriko yatatiza huduma za treni

December 5th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HUDUMA za treni kote jijini Nairobi zimefutiliwa mbali kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa ilionyesha usiku wa kuamkia Alhamisi.

Katika taarifa kwenye mitandao yake ya kijamii, kampuni ya Kenya Railways, ambayo hutoa huduma hizo kwa maelfu ya wakazi wa Nairobi, imethibitisha, “Kutokana na mafuriko katika maeneo kadhaa ya barabara zetu za reli za treni ya Nairobi, hatuna uwezo wa kutoa huduma kutoka makao makuu ya treni za Nairobi kati ya kituo kikuu na vituo vya Kikuyu, Ruiru, Embakasi na Syokimau kwa sababu za kiusalama.”

“Tunaomba wateja kutafuta njia mbadala kufika wanakoelekea. Tunashughulika kurejesha huduma hizi kwa haraka iwezekanavyo. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote ambao umetokana na hali hii,” taarifa hiyo imesema.

Wateja wengi walielekea katika vituo mbalimbali vya kuabiri garimoshi mapema Alhamisi, lakini baada ya kusubiri kwa muda na kupokea habari kuwa huduma hizo zitakosa, walilazimika kutembea kwa miguu.

Baadhi yao pia walilazimika kulipa nauli ya juu ya magari yaliyotumia fursa ya kukosekana kwa treni kuongeza nauli wanazotoza.

Kwa mfano, magari yanayohudumu barabara ya Embakasi, ambayo kwa kawaida hulipisha nauli ya kati ya Sh40 na Sh50, yaliripotiwa kupandisha hadi Sh100 yalipofahamu hakuna treni.

Kulikuwa na uhaba wa magari katika maeneo mengi yanayohudumiwa na treni, huku steji nyingi za magari zikionekana kujaa watu wakiyasubiri.

Kila siku, mji wa Nairobi unahudumiwa na treni nane zinazobeba maelfu ya watu, ambao Alhamisi walilazimika kutumia magari ama kutembea kwa miguu.