Habari Mseto

Mafuriko yatatiza wakazi wa Nyando na Taita Taveta corona ikienea

March 18th, 2020 2 min read

CECIL ODONGO na LUY MKANYIKA

WAKAZI 1,000 katika eneobunge la Nyando wameachwa bila makao baada ya nyumba zao kusombwa na maji ya mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa eneo tambare la Kano.

Maeneo yaliyoathirika zaidi yapo katika wadi ya Kabonyo Kanyagwal ambako walioathrika wamekita kambi katika kituo cha kibiashara cha Omuonyole.

Shule za msingi na za upili ya Kandaria, Ombaka na Ogenya zimejaa maji ya mafuriko japo wanafunzi hawako shuleni kutokana na agizo la serikali kwamba zifungwe ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Chifu wa Lokesheni ya Kanyagwal Boaz Nyandeje jana alieleza Taifa Leo kwamba hali inazidi kuwa mbaya kutokana na mvua hiyo ambayo imesababisha shughuli za usafiri kutatizika.

“Katika lokesheni yangu pekee wakazi 384 hawana makao. Baadhi ya familia bado zinaendelea kuokoa mali yao. Inasikitisha kwa kuwa tulikuwa katika hali hii miezi miwili iliyopita,” akasema.

“Wananchi walioathirika wamekongamana karibu na mti wa mwembe kilomita chache kutoka Ogenya. Tumepokea vyandarua kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu na tunatoa wito kwa serikali kuu na ile ya kaunti ili iwasaidie wakazi,” akasema Bw Nyandeje.

Naibu Chifu wa Ugwe, Bw George Abot naye alithibitisha kwamba watu 581 wameathirika.

Alisema kwamba wakazi hao kwa sasa wanahitaji vyakula, dawa na neti za kukinga mbu huku akihofia mkurupuko wa kipindupindu.

Mkazi wa Kandaria, Bw Cornel Ochanjo ambaye nyumba yake ilisombwa, aliomba serikali iwape msaada, ili waendelee na maisha yao kama kawaida.

“Kuna waliolazimika kuhama na sasa wamekita kambi Omuonyole, Nyang’ande huku wengine wakiishia na jamaa zao,” akasema.

Katika Kaunti ya Taita Taveta, zaidi ya familia 100 zililazimika kuhama makwao kutokana na mafuriko.

Wakazi sasa wanataka suluhu la kudumu wakisema wameteseka kila mara yanapotokea.

Jumanne, familia hizo zililazimika kutafuta hifadhi kwengine baada ya mto Njoro kuvunja kingo zake na kusababisha mafuriko hayo.

Vilevile mazao katika zaidi ekari 500, yaliharibiwa na maji, barabara nazo zikiharibika na kutatiza shughuli za usafiri.

Mkazi wa kijiji cha Kimorigo, Bw Robert Mwaiseghe alisema hali inazidi kuwa mbaya tangu mafuriko hayo yaanze wikendi.

“Baadhi ya nyumba zetu zimeharibika huku maji ya mafuriko yakisomba mimea na mali yetu. Tunahofia mkurupuko wa kipindupindu. Kinachosikitisha ni kwamba tumekuwa kwenye hali sawa na hii kila msimu wa mvua,” akasema Bw Mwaiseghe.

Mshirikishi wa shirika la msalaba mwekundu Taita Taveta Joram Oranga aliwataka waathiriwa kuhamia maeneo ya juu lakini wakalalamika kwamba ardhi hizo zinamilikiwa na watu wengine na hawana pa kujenga makazi mapya.