Habari za Kaunti

Mafuriko yavamia Msikiti wa Jamia mjini Sindo

May 16th, 2024 2 min read

WAISLAMU katika mji wa Sindo, Kaunti ya Homa Bay, wamepata pigo baada ya maji ya mafuriko kuzi msikiti wa pekee katika eneo hilo.

Msikiti huo wa Jamia upo mjini Sindo na unapatikana pembeni mwa Ziwa Victoria.

Umejaa maji kwa muda wa wiki tatu sasa.

Waislamu huswali mara tano kwa siku na kutokuwepo kwa msikiti huo sasa ni pigo wakilazimika kuswali nyumbani.

Kwa mujibu wa Imam wa msikiti huo Issa Rajab, kiwango cha maji kilianza kupanda mapema Machi.

Kufikia mwisho wa mwezi huo, maji yalikuwa yamefika kwenye ua wa msikiti.

“Maji yaliingia msikiti mnamo Aprili na tumekuwa tukizingirwa na maji kwa muda wa mwezi uliopita,” akasema Bw Rajab.

Kwa sasa hali ya sasa msikiti huo hauruhusu waumini wengi kufika na kuswali. Bw Rajab anaeleza kuwa kuna zaidi ya waumini 50 wa Kiislamu wanaotumia msikiti huo.

Hata hivyo, sasa ni waumini 20 pekee ambao wanafika kuswali na hata nafasi ya kuswali haitoshi kwa sababu wanalazimika kutumia sehemu moja ya msikiti ambao haujajaa maji.

Mara nyingine huwa wanaswali kwa awamu huku nao wazee na watoto wakiomba nyumbani pekee. Bw Rajab amesema kuwa imekuwa vigumu kutembea na kufika msikitini.

“Lazima tungeibuke na njia ya kufikia msikitini. Baadhi ya waumini huwa wanakuja na magunia wakiwa wameyajaza mchanga kisha kuyaweka katika njia ili kupita,” akaongeza Bw Rajab.

Hata hivyo, baada ya kipindi kifupi maji yalizidi na kuyafunika magunia hayo.

Hata eneo ambalo Waislamu walikuwa wakitawadhia sasa limejaa maji.

Msikiti wa Jamia mjini Sindo ukiwa umezingirwa na maji ya mafuriko mnamo Mei 15, 2024. PICHA | GEORGE ODIWOUR

Vilevile nyumba ambazo zilikuwa zikitumika na walinzi wa msikiti zimejaa maji na hata sehemu ambayo ilikuwa ikitumika kwa masomo ya madrassa, sasa inatumika kuswali.

Bw Rajab alisema kuwa sasa wapo tayari kuhamisha mskiti huo hadi eneo jingine, ambapo mafuriko hayawezi kufika. Aidha mafuriko ya sasa yameathiri masomo ya madrassa kwa watoto wadogo na kuna hofu kuwa huenda wakasahau waliyofunza.

“Tulikuwa na madrassa ya kila siku lakini sasa hayapo,” akasema,

Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Nchini (Supkem) Homa Bay Nuhu Masud alisema Waislamu wa Sindo sasa lazima wasake pahala pengine pa kuswali wakisubiri maji yapungue.

“Njia mbadala ni kuwa wawe wakiswali katika nyumba ya muumini moja siku ya Ijumaa,” akasema Bw Masud.

Kando na Waislamu wa msikiti wa Jamia, wavuvi mjini humo pia wamelalamikia kuathirika kutokana na maji mengi ya mafuriko. Wanasema maji hayo yamechangia uhaba wa samaki.

Kwa mujibu wa George Ouma, kuna uhaba wa samaki aina ya omena na sasa hilo limewaathiri kiuchumi kwa sababu mapato yao yamepungua.