Habari za Kitaifa

Mafuriko yazidi kutatiza maelfu onyo la mvua zaidi likitolewa

April 24th, 2024 2 min read

NA WAANDISHI WETU

MAELFU ya watu wanateseka kwa kufurushwa makwao huku mvua kubwa inayonyesha kote nchini ikitabiriwa kuendelea.

Mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa David Gikungu ameambia Taifa Leo mnamo Jumatano kwamba Wakenya watarajie mvua nyingi.

“Kwa kipindi cha saa 24 zilizopita, Dagoretti Corner imepata mvua ya milimita 24.5 huku Eastleigh ikipata 84.5 na Kabete 89.5. Eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) limepokea mvua ya milimita 17.5 huku uwanja wa Wilson kukishuhudiwa mvua ya milimita 51.6,” akasema Dkt Gikungu.

Mnamo Jumanne katika eneo la Syokimau, Kaunti ya Machakos wakazi walilazimika kuhama makazi yao baada ya kuzingirwa na mafuriko.

Felix Kavi ambaye anaishi katika nyumba ya makazi ya 360 ni miongoni mwa waathiriwa ambao nyumba zao zimefurika kufuatia mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa katika kaunti mbalimbali nchini.

Naye Marcella Mbithe ambaye ameishi katika eneo la Maxim tangu 1992 anasema kwamba aliamka Ijumaa na kupata nyumba yake imefurika.

“Sijawahi kushuhudia janga kama hili tangu nianze kuishi hapa. Ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya majengo katika eneo hili yana mifereji duni,” akasema Bi Mbithe.

Haya yanajiri huku viwango vya maji vikiendelea kuongezeka katika bwawa la Masinga Kaunti ya Embu.

Wanaoishi karibu na bwawa hilo wameachwa na hasara kubwa huku mazao yao, yakisombwa na maji.

“Mara nyingi huwa tunalima karibu na bwawa hasa wakati kiwango cha maji kimepungua lakini sasa tumepata hasara kubwa kutokana na mvua, mazao yetu yamesombwa na maji,” mmoja wa wakazi alisema.

Jumatano wiki jana serikali ilitoa tahadhari kwa wanaoishi karibu na bwawa la Masinga kuhama kwani kiwango cha maji katika bwawa hilo limeongezeka kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha. Bwawa hilo, hifadhi kubwa zaidi ya maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme nchini limejaa.

Katika eneo la North Rift, zaidi ya familia 400 zimekimbia makazi yao na hekari kadhaa za mazao ya chakula kuharibiwa. Mafuriko hayo pia yameharibu barabara na miundombinu na kuzorotesha huduma za usafiri katika maeneo kadhaa ya mkoa huo.

Mali ya thamani isiyojulikana pia imeharibiwa na mafuriko katika maeneo mbalimbali ya kaunti za Turkana, Pokot Magharibi, na Elgeyo Marakwet huku mabwawa na mito yakipasua kingo, huku idara ya hali ya hewa ikionya kuwa mvua itaendelea kunyesha.

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini na serikali za kaunti katika eneo hilo zinasambaza vifaa vya matibabu na dawa kwa familia zilizoathiriwa ili kukabiliana na mlipuko wa magonjwa kama vile malaria.

Katika Kaunti ya Turkana, wakazi wamepata hasara huku mafuriko ya Ziwa Turkana yakileta uharibifu. Ziwa hilo limefurika na hivyo kuweka maisha ya mamia ya wanakijiji wanaolitegemea kwa samaki katika hatari kubwa.

“Nyumba 76 zimeathiriwa na mafuriko katika mji wa Lodwar katika muda wa saa 24 zilizopita huku baadhi ya mabwawa na mito katika eneo hilo yakivunja kingo kutokana na mvua kubwa inayoendelea,” alieleza meneja wa Shirika la Msalaba Mwekundu wa North Rift, Oscar Okumu akiongeza kuwa familia 360 zimeathiriwa na mafuriko Lodwar, Kaunti ya Turkana, na zinahitaji chakula cha misaada.

Ripoti za: Daniel Ogetta, Simon Ciuri, Sammy Lutta, Barnabas Bii, Evans Jaola, George Munene, Sammy Kimatu, Waikwa Maina na Geoffrey Ondieki