Makala

Mafuriko yasaidia kufungia magaidi njia ya kufikia raia

June 12th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

JAPO mafuriko husababisha maafa na hasara katika maeneo mbalimbali nchini, katika baadhi ya sehemu kwenye Kaunti ya Lamu huwa yanageuka kiokozi kwa kufungia magaidi mwanya wa kupenya kushambulia wasafiri barabarani.

Sehemu kama vile Gamba, Nyongoro, Lango la Simba, na Kona Mbaya, ambazo zinatambulika kwa visa vya magaidi kujitokeza ghafla barabarani na kuua wapita njia huwa zimejaa maji, hivyo kuwakosesha magaidi hao nafasi wakati kukiwa na mafuriko.

Hata vizuizi vya walinda usalama huwa vimepungua sehemu hizo kwa wakati huo na kuwekwa maeneo ambayo yako wazi.

Sehemu mojawapo ya barabara kuu ya Lamu-Garsen ikiwa imejaa maji ya mafuriko. Maji ya mafuriko kandokando mwa barabara hiyo yamekuwa yakiziba mianya ya magaidi, hasa Al-Shabaab kupenya kuvamia wapita njia. PICHA | KALUME KAZUNGU

Visa vya magaidi wa Al-Shabaab kuwalenga, kuwashambulia, kuwajeruhi au hata kuwaua wapita njia kwenye barabara kuu ya Lamu-Garsen vimekuwepo kwa muda mrefu.

Magaidi hujitokeza barabarani ghafla na kutekeleza mashambulio kwa wasafiri.

Mbali na maeneo yaliyotajwa mwanzo, pia Mwembeni, Mambo Sasa, na Milihoi hulengwa.

Yaani sehemu hizi zimekuwa zikivuma kutokana na ukatili ambao magaidi wamekuwa wakiutekeleza kwa watumiaji wa barabara.

Ni sehemu ambazo licha ya kulindwa kila mara na karibu saa zote na polisi au Jeshi la Ulinzi Kenya (KDF), Al-Shabaab bado wamekuwa wakipata mwanya na kupenya kuja kuvamia raia, kuwajeruhi au hata kuwaua.

Washambuliaji hutekeleza ukatili wao kupitia kuwapiga risasi au kuwachinja na kisha kurudi vichakani. Maafisa hupambana lakini katika baadhi ya visa, Al-Shabaab hutokomea msituni wasikamatwe.

Makumi ya visa vya wasafiri kushambuliwa, ama wawe ni abiria walioabiri mabasi ya usafiri wa umma, magari ya kibinafsi au hata walinda usalama vimeripotiwa kwenye maeneo hayo.

Kwa mfano, mnamo Agosti 21, 2023, watu wawili, akiwemo dereva wa lori na msaidizi wake, waliuawa kwa kuchinjwa pale magaidi wanaoaminika kuwa wa Al-Shabaab walipojitokeza barabarani eneo la Lango la Simba, ambapo waliwalazimisha wawili hao kusimama ambapo waliwaamuru kushuka chini na kisha kuwachinja.

Baadaye waliliteketeza lori lao ambalo walikuwa wakisafirishia mchanga wa kujengea kutoka Malindi kuelekea Lamu.

Mnamo Agosti 1, 2023, watu wawili, akiwemo mke wa diwani wa wadi ya Hindi, Kaunti ya Lamu, Bw James Njaaga, waliuawa kwa kupigwa risasi huku wengine 10, akiwemo diwani mwenyewe, wakijeruhiwa vibaya magaidi walipovamia magari ya wapita njia kwenye eneo la Mwembeni kati ya Lango la Simba na Nyongoro kwenye barabara hiyo kuu ya Lamu-Garsen.

Magari na pikipiki pia zilichomwa kwenye uvamizi huo wa asubuhi.

Jambo la kutia moyo, hasa miaka ya hivi punde ni kwamba kila mara mafuriko yanaposhuhudiwa nchini hadi kusababisha maeneo ya barabara kuu ya Lamu-Garsen, hasa Gamba kukatika, sehemu zote ambazo magaidi huzilenga pia husombwa na mafuriko hayo.

Janga hilo la mafuriko kwa upande mwingine au kwa kiwango fulani, limekuwa likionekana au kugeuka kuwa kiokozi kwa kufungia magaidi mwanya wa kupenya kushambulia wasafiri barabarani.

Yaani kimsingi ni kuwa mafuriko, hasa yale yanayoshuhudiwa kandokando ya barabara kuu ya Lamu-Garsen, yamekuwa yakisaidia pakubwa kwa kuwafungia magaidi njia ya kufikia raia.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa hata vizuizi vya walinda usalama wakati mafuriko yanaposhuhudiwa hupunguzwa kwenye sehemu husika, ambapo badala yake maji huwa yamezagaa, hivyo kugeuka kuwa kinga madhubuti.

Baadhi ya walinda usalama waliozungumza na Taifa Leo walishukuru jinsi maji ya mafuriko ambayo mara nyingi huwa yamezagaa na kutwaa sehemu kubwa za kandokando ya barabara.

“Sehemu zenyewe ambazo maji huwa yamezagaa ni zile zinazotambulika kuwa hatari kwa kulengwa na magaidi. Hao Al-Shabaab hufungiwa kabisa na hayo maji ya mafuriko kiasi kwamba huwa hawana mwanya wa kujipenyeza kufikia sehemu yetu ya barabara kutekeleza mashambulizi,” akasema mmoja wa walinda usalama aliyedinda kutaja jina lake kutokana na kwamba hajapewa mamlaka rasmi ya kuzungumza na vyombo vya habari.

Maafisa hao wa usalama walisema mafuriko yamesaidia kurahisisha majukumu yao kwa kiwango fulani.

Wanasema kila kunaposhuhudiwa mafuriko wao huishia kuweka vizuizi vyao vya kuwapekua wasafiri na kudhibiti usalama kwenye sehemu ambazo ziko wazi pekee ilhali sehemu zingine maji yakiwa yametapakaa au ‘kushika doria’ kimpango.

“Ni hali ambayo imesaidia sisi walinda usalama pakubwa, hasa wakati tukitekeleza doria zetu kwani tumekuwa tukiweka vizuizi vichache ilhali sehemu zingine vizuizi vikiwa ni maji tu,” akasema afisa mwingine.

Wasafiri waliohojiwa pia hawakuficha furaha yao kwamba hata visa vya mashambulio ya Al-Shabaab hupungua nyakati za mafuriko.

“Ni dalili tosha hayo mafuriko yanawakabili na hata kuwatokomeza mbali magaidi kimpango. Wiki zote za mafuriko huwa hatushuhudii mashambulio au majaribio yoyote ya mashambulio kutoka kwa Al-Shabaab. Watafikaje barabarani kushambulia ikiwa sehemu nyingi za kandokando ya barabara yetu zimesombwa na mafuriko? Yaani mafuriko kwetu sisi wakazi wa Lamu ni mibaraka kwa kiwango fulani,” akasema Bw Said Mohammed, msafiri wa kila mara kwenye barabara kuu ya Lamu-Garsen.

Wasafiri hata hivyo walichacha kwa walinda usalama kutopuuza hizo sehemu zenye mafuriko ya kandokando ya barabara.

Bi Maryam Ahmed alisema ni vyema vizuizi vya walinda usalama viendelee kuwepo hata kwenye yale maeneo yenye mafuriko ili kuwahakikisha wasafiri usalama wao.

“Hata ikiwa kila mafuriko yanaposhuhudiwa magaidi hawashambulii lakini hilo halimaanishi tupuuze sehemu hizo mbaya. Vizuizi vya polisi na jeshi viendelee kuhudumu kama kawaida. Kamwe huwez kutabiri yalivyo ya kesho. Hawaaminiki hao maadui na wala huwezi kutabiri mienendo yao,” akasema Bi Ahmed.

Mbali na mafuriko kuwa na tabia ya kusomba na kuziba kabisa maeneo hayo ya barabara yavumayo kwa mauaji ya Al-Shabaab, serikali kuu pia mnamo 2018 ilibuni kambi za kudumu za polisi na jeshi kwenye sehemu hizo husika.

Hatua hiyo ilichukuliwa kama njia mojawapo ya kudhibiti usalama ya watumiaji wa barabara hiyo kuu baada ya visa vya magaidi kuua watumiaji wa barabara hiyo kukithiri miaka ya awali.