Habari Mseto

MAFUTA: Gharama ya maisha kupanda zaidi

May 14th, 2019 2 min read

Na BERNARDINE MUTANU
WAKENYA wanatarajiwa kukumbana na hali ngumu ya maisha kwa kipindi cha mwezi mmoja ujao, baada ya Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) kutangaza jana bei mpya ya mafuta inayoongezeka kwa zaidi ya shilingi tano.
Kwenye taarifa ya kubadilisha bei za mafuta ya petrol, dizeli nay ale ya taa ERC ilieleza kuwa imesukumwa kuchukua hatua hiyo kwa sababu ya kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo muhimu katika soko la kimataifa.
Inakadiriwa kuwa ongezeko hilo huenda likaathiri bei za bidhaa muhimu zinazotegemea mafuta, mbali na kushuhudiwa kupanda kwa nauli.
Katika mabadiliko hayo, mafuta ya petroli yalipanda kwa Sh5, dizeli kwa Sh2 na mafuta taa kwa zaidi ya Sh2.
“Ongezeko la bei mwezi huu ni kutokana na ongezeko la bei ya mafuta yaliyoagizwa, ambapo bei ya petroli iliongezeka kwa asilimia 11.39 kutoka Sh62,054 kwa tani mwezi Machi hadi Sh69, 125 kwa tani,” ilisema ERC katika taarifa iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mkuu Bw Pavel Oimeke.
Tani moja ya dizeli iliongezeka kwa asilimia 2.75 kutoka Sh62, 451 hadi Sh64, 167 kwa tani moja ilhali bei ya mafuta taa iliongezeka kwa asilimia 2 kwa tani kutoka Sh66, 255 hadi Sh67, 582.
Ongezeko hilo pia lilitokana na kudhoofika kwa sarafu ya Kenya dhidi ya Dola ya Amerika kwa asilimia 0.65 kutoka Sh100.47 dhidi ya Dola mwezi Machi na kufikia Sh101.12 dhidi ya Dola mwezi huu wa Aprili.
Mjini Mombasa, mafuta aina ya petroli yatauzwa kwa Sh109.38, dizeli Sh101.75 na mafuta taa Sh101.99 kwa mwezi mmoja ujao kuanzia Mei 15.
Nairobi petrol itauzwa Sh112.03 kwa lita, dizeli Sh104.37 huku mafuta ya taa yakipatikana kwa Sh104.62 kwa lita.
Mnamo Septemba mwaka jana, Wakenya walilalamikia kuanza kutekelezwa kwa sheria ya kutoza bidhaa za mafuta kodi ya asilimia 16. Wabunge kupitia Mswada wa Fedha walipendekeza ushuru huo uahirishwe, lakini badala yake Rais Uhuru Kenyatta alipunguza kodi hiyo kwa asilimia 8.
Japokuwa bei ya mafuta ilipungua mwishoni mwa Februari na kufikia hata Sh99 kwa lita jijini Nairobi, inaonekana serikali imeanza upya kuongeza kidogo kidogo ushuru huo ili kurejesha ulipodhamiriwa.