Kimataifa

Mafuta ya kubadili rangi ya ngozi yaondolewa madukani Rwanda

January 8th, 2019 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

SERIKALI ya Rwanda imeanza kutekeleza marufuku kwa bidhaa za mafuta na sabuni za kubadili rangi ya ngozi, baada ya bidhaa hizo kuanza kuondolewa madukani, kufuatia kutangazwa kwa marufuku hiyo Novemba 2018.

Tangu marufuku hiyo ilipotangazwa, serikali imekuwa ikivamia maduka yanayouza bidhaa hizo na kuzinyakua, sasa hali ikizidi kwani wafanyabiashara wenyewe wanaziondoa wasipatikane.

Kuungwa mkono kwa marufuku hiyo na Rais Paul Kagame kumeipa serikali nguvu ya kuitekeleza, japo Wanyarwanda wengi wameibua pingamizi.

Rais huyo alilazimika kumjibu raia wake mmoja aliyeibua malalamishi kwenye akaunti yake ya Twitter, akisema si salama kiafya kwa watu kutumia mafuta hayo.

“Si salama kiafya pamoja na mambo mengine. Inahusisha matumizi ya kemikali ambazo zimepigwa marufuku. Wizara ya afya na idara ya usalama zinafaa kuchukua hatua ya mara moja,” Rais Kagame akasema.

Madini ya zaibaki yanasemekana kupatikana katika bidhaa nyingi hizo za kubadili rangi ili watu wawe weupe, ambayo wanawake wengi wa Kiafrika wamekuwa wakichangamkia.

Ni madini hayo ambayo yanasemekana kuwezesha ngozi ya mtumizi kubadilika na kuleta weupe unaohitajika, wengi wakitamani mafuta hayo.

Hata hivyo, madini hayo ni hatari kwa afya kwani yanaweza kuadhiri kibofu ama ini la mtumizi, ama kusababisha saratani ya ngozi.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), takriban mwanamke mmoja kati ya kila wanne wa Afrika hutumia bidhaa za kubadili rangi.