Kimataifa

Mafuta ya kuimarisha urembo yamfurisha uso

November 30th, 2018 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

MWANAMKE mmoja amedai kuwa alikuwa karibu kufa alipotumia mafuta ya kubadili rangi ya nywele lakini yakaharbikiangozi yake na kufanya ukubwa wa kichwa chake kuongezeka mara mbili.

Mwanamke huyo wa miaka 19 kwa jina Estelle na ambaye ni mwanafunzi Jijini Paris, Ufaransa alichapisha picha za kuogofya kuonyesha namna alibadilika kuwa baada ya kutumia kemikali aina ya PPD (Paraphenylenediamin) ambayo kwa kawaida hupatikana katika maduka ya bidhaa za urembo.

Alikuwa amenunua mafuta hayo katika duka la jumla awali mwezi huu na kuyatumia alipofika nyumbani namna maelekezo kwenye mafuta hayo yalivyosema.

Hata hivyo, badala ya kufunika kichwa kwa saa 48 kama maelekezo kwenye mafuta yalivyosema, alisubiri kwa dakika 30 pekee. Alianza kusikia mwasho kichwani kisha akaanza kufura.

Alijaribu kutumia dawa lakini siku iliyofuata alipata kuwa hali ilikuwa imeharibika, kichwa chake kikifura kufikia sentimita 63.

Mwanafunzi huyo alieleza shirika moja la habari kuwa alishindwa kupumua na kuwa kichwa chake “kilikuwa chepesi kama balbu.”

Hata alipokimbizwa hospitalini, ulimi wake pia uliendelea kufura.

Ijapokuwa sasa amepona, anasema bado anaona alama za kufura, huku akikiri kuwa ‘alifanya kosa’ alipofanya jaribio kuona ikiwa mafuta hayo yangeadhiri ngozi yake, sasa akitaka kuwaonya watu wengine kuhusu hatari ya kemikali ya PPD.

“Nilikuwa karibu kufa, sitaki hilo limfanyikie mtu mwingine,” mwanamke huyo akaeleza wanahabari.

Mafuta ya kubadili rangi huwa na kemikali tofauti lakini PPD ndiyo huadhiri ngozi zaidi mtu anapoipaka nywele.