Habari Mseto

Mafuta ya upako yakosa kumwepushia mhubiri kifungo cha maisha

August 17th, 2018 2 min read

Na TITUS OMINDE

MAFUTA ya upako ambayo pasta mmoja alifika nayo mahakamani mjini Elodret hayakumsaidia kuepuka kifungo cha maisha, baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi mtoto wa miaka mitano.

Mtumishi huyo wa kanisa la SDA ambaye alikuwa akihudumu kama mchungaji katika shule ya Kiadventisti ya Kabote, Kaunti ya Nandi, alisababsiha kioja mahakamani pale alipoanza kunyunyiza mafuta hayo kortini wakati wa kutolewa hukumu.

Kwa wakati mmoja jaji alisitisha kusoma hukumu hiyo huku akitaka maafisa wa usalama kortini kumtaka mshtakiwa aachane na kitendo hicho.

Mshtakiwa huyo amekuwa nje kwa dhamana.

Licha yake kuamini kuwa mafuta ya upako yangempa afueni dhidi ya kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi mtoto wa miaka mitano ambapo mahakama ya hakimu mwandamizi mjini Kapsabet ilikuwa imemhukumu kifungo cha maisha.

Tom David Orwaru Nyakundi ambaye alikuwa amehukumiwa kifungo hicho na mahakama ya Kapsabet mnamo Juni 20 mwaka 2013, alikwa amekata rufaa dhidi ya hukumu hiyo katika mahakama kuu ya Elodret kupitia kwa wakili wake Annasi Momanyi.

Awali mahakama iliambiwa kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo mnamo Julai 8 mwaka 2012 katika kijiji cha Kipsebwo, Kaunti ya Nandi.

Katika rufaa yake aliwasilisha hoja 16 za kupinga uamuzi wa kumfunga maisha uliotolewa na hakimu mwandamizi wa Kapsabet.

Miongoni mwa masuala ambayo aliwasilisa mahakamani yalikuwa ukosefu wa ushahidi wa kutegemewa kwa upande wa mlalamishi ikizingatiwa kuwa umri wake ulikuwa mdogo sana.

Vilevile alikosoa mahakama hiyo kwa kukosa kubaini umri wa mlalamishi kwa kutumia cheti cha kuzaliwa au kumpima umri kupitia kwa mtaalam wa afya ambaye amehitimu miongoni mwa vigezo vingine.

Mshtakiwa aliambia mahakama kuu kuwa hakimu wa mahakama ya chini alitoa uamuzi wake kimapendeleo ambapo alimpa kifungo kikali.

Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita akiwemo mlalamishi ambaye alimtambua mshtakiwa.

Mahakama iliambiwa kuwa mshtakiwa alimnajisi mtoto huyo nyumbani kwake kwani walikuwa wamejuana kama majirani na kuzoeana.

Hata hivyo, jaji Olga Sewe alimwondolea hakimu wa mahakama ya chini lawama dhidi ya uamuzi wake huku akisema kuwa kifungo hicho kilistahili.

Katika uamuzi wake, alisema kuwa aliridhika na hukumu na kifungo hicho kwa mujibu wa sheria za unajisi watoto katika ibara ya 8(1) na 8(2) mtawalia.

“Kutokana na ushahidi ambao umewasilishwa na upande wa mashtaka kupitia kwa mashahid sita, ninaidhinisha kifungo hicho huku nikitupilia mbali rufaa ya mshtakiwa,” aliamuru jaji huku akitoa hukumu ya maisha kwa mtumishi wa Mungu.