DCI yatahadharisha al-Shabaab imetuma magaidi kushambulia

DCI yatahadharisha al-Shabaab imetuma magaidi kushambulia

BENSON MATHEKA MARY WAMBUI

IDARA ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) imetoa majina na picha za washukiwa wanane hatari wa kundi la Al Shabaab waliopatiwa mafunzo Somalia, na kutumwa Kenya kutekeleza mashambulizi ya kigaidi.

Kwenye taarifa, idara hiyo ilisema kwamba baadhi ya washukiwa hao wako na silaha na kuomba umma kutoa habari zitakazosaidia kuwakamata.

“DCI inaomba umma kutoa habari zinazoweza kusaidia kukamatwa kwa washukiwa hawa wanane wa ugaidi, wanaohusishwa na mtandao wa al-Shabaab,” alisema Mkurugenzi wa DCI, George Kinoti kwenye taarifa kupitia mitandao ya kijamii.

Washukiwa hao ni Mohammed Ali Hussein na Ahmed Ali Mohamed ambao ilisemekana walitoroka baada ya kukamatwa eneo la Merti, kaunti ya Isiolo mwaka wa 2018 walipokuwa wametumwa kutekeleza shambulizi wakitumia gari lililojazwa vilipuzi.

Abdurahman Hija kwa jina jingine Mnubi, kutoka kaunti ya Nyeri inasemekana alikuwa mwanachama wa genge la wahalifu waliokuwa wakihangaisha wakazi wa mji wa Nyeri kabla ya kutorokea Somalia mwaka wa 2016 kujiunga na Al Shabaab kupata mafunzo na kutumwa Kenya kutekeleza mashambulizi.

DCI ilisema kwamba mshukiwa mwingine, Eric Njoroge Wachira anayejulikana kwa jina Mohamed Njoroge au Moha, pia ni mkazi wa kaunti ya Nyeri aliyekuwa mwanachama wa genge ya wahalifu waliokuwa wakihangaisha wakazi wa kaunti ndogo za Mukurwe-ini na Karatina kabla ya kujiunga na Al shabaab mwaka wa 2016.

Idara hiyo ilisema kuwa mshukiwa mwengine Abdikadir Mohamed Abdikadir anayefahamika kama Ikrima au Ikram au Ukasha au Abdulqadir Mahmud Ahmed au Abu Abdalla Hamisi, ni msomali na mshirika wa karibu wa viongozi wa Al shabaab wakiwemo Fazul Abdullah Mohammed, Abdi Godane na Salim Swaleh Nabhan na anatafutwa kwa kupanga shambulizi katika hoteli ya Dusit D2 Complex, Nairobi miaka mitatu iliyopita. Inasemekana amewahi kuishi mitaa ya South C , Nairobi na Kongowea/Nyali kaunti ya Mombasa.

Bw Kinoti alisema mshukiwa mwingine anayesakwa ni Peter Gichungu Njoroge anayefahamika kwa jina jingine Mustafa (33) aliyehitimu na digrii katika tekinolojia ya habari na mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Kisayansi na Tekinolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Alikamatwa akiwa Mandera akielekea Somalia kujiunga na Al Shabaab Julai 6 2016 na baadaye kuachiliwa kisha akaenda Somalia akiandamana na mpenzi wake Miriam Hamisi kutoka Bamburi, Mombasa. Naye

Kulingana na DCI, mshukiwa Mophamud Abdi Aden almaarufu Mohamed Yare au Ibrahim au Mohamed Hassan aliye pia na jina jingine Mohamud Abdirahman ni mmoja wa waliopanga shambulizi katika hoteli ya Dusit 2019.

Idara hiyo ilitaja mshukiwa wa nane kama Kassim Musa Mwarusi au Abu Miki aliyekuwa mkazi wa Ukunda, Kwale ambapo alikuwa mwanachama wa genge lililohangaisha wakazi wa Pwani Kusini.

You can share this post!

Ruto aambia wapinzani waache vitisho

TUSIJE TUKASAHAU: Chokoraa wangali tishio la usalama

T L