Magari matatu ya Sh13 milioni kila moja kutumiwa na madereva chipukizi Safari Rally

Magari matatu ya Sh13 milioni kila moja kutumiwa na madereva chipukizi Safari Rally

Na GEOFFREY ANENE

CHIPUKIZI McRae Kimathi, Hamza Anwar na Jeremy Wahome wataendesha magari mapya kabisa ya Ford Fiesta katika Mbio za Dunia za Safari Rally mnamo Juni 24-27.

Magari hayo ya Wakenya hao wamewasili kutoka nchini Poland. Yanagharimu Sh13 milioni kila moja.

Madereva hao wamepata udhamini muhimu Jumanne wa jumla ya Sh15 milioni.

Wanaamini usaidizi wanaopata sasa hivi utawasaidia kukuza talanta yao pamoja na kupeperusha bendera ya Kenya na Afrika kimataifa.

Dereva Hamza Anwar (kushoto) na mwelekezi wake ugani Kasarani. Picha/ Geoffrey Anene

Pia, Safaricom ilitangaza Sh2.5 milioni zitatumiwa kwa helikopta yake wakati wa mashindano hayo yatakayoanzia nje ya jumba la KICC mnamo Juni 24 na kufanyika katika eneobunge la Naivasha hapo Juni 25-27.

Katika hafla ya uzinduzi wa udhamini huo, Waziri wa Michezo Amina Mohamed alipongeza Safaricom na kampuni nyingine za kibinafsi kwa ushirikiano akisema umewezesha Safari Rally na michezo mingine kufanyika na kukuwa. Waziri huyo aliwasili katika hafla hiyo akiwa amebebwa kwa ndege iliyokodishwa kwa Sh200,000 kwa saa.

Alifichua kuwa kazi kubwa ya kuhakikisha Safari Rally inarejea katika ratiba ya dunia ilifanywa na Rais Uhuru Kenyatta. Kenya ilipoteza haki za kuandaa duru hiyo ya dunia mwaka 2003 kutokana na ukosefu wa fedha, miongoni mwa sababu nyingine.

Safaricom pia yawapa udhamini wa Sh15 milioni

Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom Peter Ndegwa alitoa hakikisho kuwa kampuni hiyo itaendelea kusaidia michezo ikiwemo gofu na soka ya mashinani na kitaifa.

Waziri wa Michezo Amina Mohamed (kushoto), Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom Peter Ndegwa na rais wa Shirikisho la Mbio za Magari za Kenya Phineas Kimathi ugani Kasarani wakati wa Safaricom kutangaza udhamini kwa chipukizi. Picha/ Geoffrey Anene

Rais wa Shirikisho la Mbio za Magari za Kenya, Phineas Kimathi alipongeza Safaricom kwa mchango wake wa kuinua chipukizi hao kuwa nyota wa siku za baadaye.

Alisema madereva hao watatu, ambao majuzi pia walipata udhamini wa Sh10 milioni kutoka kwa kampuni ya ndege ya Kenya Airways watapata mafunzo ya hali ya juu barani Ulaya baadaye mwaka huu 2021.

Dereva Jeremy Wahome. Picha/ Geoffrey Anene

Kampuni nyingine zilitotangaza kupiga jeki Safari Rally hapo awali ni pamoja na Toyota Kenya (Sh30 milioni) na benki ya KCB (Sh100 milioni) na serikali.

Dereva McRae Kimathi. Picha/ Geoffrey Anene

Toyota pia imetoa magari mawili yatakayotangulia barabarani kuhakikisha barabara za mashindano ziko salama kwa kuonya mashabiki na madereva. Nayo kampuni ya kamari ya Betika imedhamini madereva Hussein Malik, Rehan Shah, Andrew Muiruri na Maxine Wahome na waelekezi wao Shantal Young, Harshil Limbani, Edward Njoroge na Linet Ayuko kwa kima Sh80 milioni.

Safari Rally inarejea kwenye ratiba ya dunia ya WRC baada ya miaka 19. Madereva 58 wakiwemo masupastaa kutoka Ulaya kama Sebastien Ogier watawania ubingwa wa Safari Rally ambayo ndiyo duru pekee barani Afrika kwenye WRC.

Duru nyingine za dunia zilizoandaliwa ni Monaco (Januari), Finland (Februari), Croatia (Aprili), Ureno (Mei) na Italia (mapema Juni). Baada ya Safari Rally itakayofanyika katika kaunti za Nairobi, Kiambu na Nakuru, kuna Estonia (Julai), Ubelgiji (Agosti), Ugiriki (Septemba), Finland (Oktoba), Uhispania (Oktoba) na Japan (Novemba).

You can share this post!

AKILIMALI: Ufugaji wa samaki bila gharama kubwa

Wanafunzi watatu wa Thika School for the Blind ni wajawazito