Habari Mseto

Magari ya kifahari yaharibika baada ya kuangukiwa na mti Serena

March 18th, 2018 2 min read

Na BERNADINE MUTANU

Waendeshaji saba wa magari ya kifahari walioegesha magari yao katika maegesho ya Hoteli ya Serena, Nairobi, wanakadiria hasara kubwa baada ya magari yao kuangukiwa na miti.

Kisa hicho kilitokea wakati wa mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha Nairobi Jumamosi adhuhuri. Baadhi ya magari yaliyoharibiwa yalikuwa ya thamani kubwa kulingana na mkuu wa polisi katika Kituo cha Polisi cha Kilimani, Joseph Muthee.

“Hakuna aliyeumia wakati wa kisa hicho kwa sababu hakuna yeyote aliyekuwa ndani,” alisema.

Gari hili ani miongoni mwa magari saba yaliyongukiwa na mti mkubwa katika Hoteli ya Serena jijini Nairobi Machi 17, 2018. Picha/ Hisani

Baadhi ya magari hayo yalikuwa ya wahudumu katika hoteli hiyo na mengine yalikuwa ya wateja wao. Yaliondolewa baada ya mvua kupungua.

Mvua hiyo pia ilisababisha uharibifu mkubwa Nairobi ambapo watu walipoteza mali yao baada ya kusombwa na mafuriko.

Baadhi ya manyumba katika maeneo kadhaa Nairobi yaliingia maji wakati wa mafuriko yaliyofuatia.

Idara ya Utabiri wa Hewa imeendelea kuonya kuwa mvua itaendelea kuwa nyingi mwezi huu.

Gari hili aina ya Toyota Prado liliangukiwa na mti mkubwa katika Hoteli ya Serena jijini Nairobi Machi 17, 2018. Picha/ Hisani

Hilo lilitokea saa kadhaa baada ya jumba kubomoka Ruai kwa sababu ya mvua. Mtu mmoja aliokolewa na wengine wawili walisemekana kukwama ndani ya vifusi vya jumba hilo.

Tayari serikali imewataka wakazi wa Nairobi wanaoishi katika mitaa duni ndani ya majumba yaliyochorwa alama za ubomoaji kuhama kuepuka mikasa kama huo.

Serikali ya Kaunti ya Nairobi ikishirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Miji imetenga Sh194 milioni kukabiliana na mafuriko Jijini.

Waziri wa Barabara na Muundo msingi katika Jiji la Nairobi Mohamed Dagane alisema kaunti hiyo itatumia Sh32 milioni kuimarisha mfumo wa upitishaji wa maji katika Kaunti ya Nairobi na kukabiliana na athari za mvua.

Mti huu uliangukiwa magari saba katika Hoteli ya Serena jijini Nairobi Machi 17, 2018. Picha/ Hisani

Alisema kuwa serikali ya kaunti ilikuwa inatambulisha maeneo ambayo huathiriwa zaidi na mafuriko. Alisema tayari imezindua program dhabiti ya kukabiliana na mafuriko ya ghafla.

Serikali hiyo itaanza ujenzi wa mfumo wa kupitisha maji taka na kurekebisha mabomba ya maji taka kote jijini.

Barabara zilizolengwa kwa marekebisho ya mitaro na mabomba ya kupitisha maji taka ni Catherine Ndereba, Lang’ata South, Kayole Spine, Popo, Mai Mahiu, Macharia, barabara ya Kawangware 46-Muslim Primary School, na Jonathan Ng’eno .