Habari Mseto

Magari ya uchukuzi yanayohudumu baina ya Githurai na Nairobi kuhamia stendi mpya

June 27th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

MAGARI ya uchukuzi wa umma yanayohudumu baina ya maeneo ya mtaa wa Githurai na jiji la Nairobi yatahamia katika stendi mpya, eneo la Githurai lililoko Kaunti ya Kiambu.

Hii ni kufuatia ukarabati wa eneo linalolengwa kuwa stendi, unaoendelea chini ya ufadhili wa serikali ya kaunti hiyo.

Mabasi yanayohudumu eneo hilo yamekuwa yakibebea abiria pembezoni mwa Thika Superhighway, na mengine kuegeshwa barabarani, jambo linalochangia kuwepo kwa msongamano.

“Ukarabati huu umekuwa ukiendelea kwa muda wa wiki kadhaa,” mmoja wa wafanyakazi wanaoendeleza shughuli hiyo ameambia Taifa Leo.

Eneo hilo linakarabatiwa kwa kuwekwa mawe na udongo kabla ya hatua za kumalizia.

“Tunaona ukaratabati ukiendelea. Tumeskia huenda tukahamishiwa humo, ingawa haijakuwa rasmi na wakati tutakaohamia,” amesema mhudumu mmoja wa matatu.

Mwaka wa 2018 mabasi hayo yalikuwa yameondolewa yanakohudumia kufuatia shinikizo la halmashauri ya barabara kuu nchini, KeNHA.

Aidha, yalikuwa yakibebea eneo linalokarabatiwa lakini wahudumu walilalamikia abiria kuhangaika kujua yaliko matatu.

Ni katika eneo hilo, lililopakana na soko la Githurai na ambalo 2018 na 2019 vibanda vya wafanyabiashara vilibomolewa.

Ujenzi wa soko litakalohamishiwa wafanyabiashara hao unaendelea.