Habari za Kitaifa

Magari ya umeme kuwa na nambari maalum

March 29th, 2024 1 min read

NA HILARY KIMUYU

SERIKALI imetangaza kwamba magari yanayotumia Umeme (EVs) sasa yatakuwa na nambari spesheli za usajili zenye rangi ya kijani.

Tangazo hilo lilitolewa na Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen, wakati wa uzinduzi wa rasimu ya sera ya vyombo vya uchukuzi vinavyotumia stima katika Jumba la KICC.

Waziri Murkomen alisema nambari hizi za kipekee zitatolewa kwa madereva wanaomiliki magari yanayotumia umeme sawia na pikipiki, kuashiria nchi kupiga hatua katika safari ya sekta ya uchukuzi.

“Nambari mpya za usajili wa magari hayo maalum zitasaidia kuhamasisha na kuhimiza watu zaidi kufikiria kuhamia katika mfumo wa utumiaji wa magari na pikipiki za kutumia stima,” Bw Murkomen akasema.

Aidha, waziri Murkomen alisema kuwa mpango huo utatumika pia kwa pikipiki, kuashiria juhudi kubwa za kuleta mabadiliko katika sekta ya uchukuzi nchini.

Bw Murkomen aliongeza kuwa hatua hiyo ni ya faida kwani itapunguza pakubwa utoaji wa hewa chafu huku ikipunguza gharama ya uagizaji mafuta.

“Kuhamia kwa magari ya umeme (EVs) hupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa chafu huku ikipunguza fhrama ya uagizaji wa petroli, ambao kwa uwepo wa nafasi za kazi. Ndiyo maana Serikali imeweka kipaumbele katika kukumbatia EVs,” alisema.