Habari MsetoSiasa

Magavana 10 sasa walenga urais na useneta 2022

May 6th, 2018 2 min read

Na JUSTUS WANGA

MAGAVANA 10 wanaohudumu kwa kipindi cha pili na cha mwisho tayari wameanza kuweka mikakati kuhusu maisha yao ya kisiasa baada ya 2022.

Huku wachache kama Hassan Joho, 45, (Mombasa) na Alfred Mutua, 47, (Machakos) wakielekeza macho yao katika kiti cha urais, sehemu kubwa ya waliosalia wanawazia kujitosa katika kinyang’anyiro cha Useneta ama ‘Nyumba ya Wazee’ – kama ambavyo imerejelewa na wabunge kadha wa kitaifa katika vuta nikuvute zao za kuonyesha ubabe baina yao na maseneta.

Magavana wamelazimika kuanza kujipanga kutokana na Kifungu 180 (7a) cha Katiba kinachowazuia kuwania tena kiti hicho baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili mtawalia.

Sharti hilo halizingatii umri wala umaarufu wa gavana.

Ni hali halisi ambayo imewapiga kumbo magavana hao ambao wamelazimika kuanza kujitayarisha kwa maisha ya baadaye ya kisiasa miezi kadha baada ya kutetea viti vyao na miaka minne kabla utawala wao kukoma.

Ukweli mwingine mchungu kwa wale wanaomezea mate kiti cha urais ni kwamba, ingawa mfumo wa ugatuzi unaruhusu ‘marais wadogo’ 47 ni mmoja pekee anaweza kuwa kiongozi wa taifa, jambo ambalo limefanya kinyang’anyiro cha urais kuwa na ushindani mkali.

Gavana mchanga kabisa ni Alex Tolgos, 38, wa Elgeyo Marakwet na duru zinasema anawazia kuingia Seneti.

Wandani wake wanasema kuna uwezekano wa ‘kubadilishana’ viti na Kiongozi wa Wengi Seneti Kipchumba Murkomen, ingawa seneta huyo amewadokezea marafiki wa karibu nia yake ya kuendelea kushikilia wadhifa muhimu katika serikali ya Naibu Rais William Ruto iwapo atafanikiwa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Baadhi ya wakuu hao wa kaunti wanalenga nyadhifa za ubalozi na uwaziri katika serikali ijayo.

Mahojiano na wengi wao yamedhihirisha jinsi hawana haja ya kung’ang’ania viti vya ubunge kutokana na hadhi ya kiti cha ugavana pamoja na fedha nyingi ambazo magavana husimamia.

Gavana Joho asema ananuia kuwania urais kwa tiketi ya chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga.

“Nitafika kila pembe ya nchi kuomba kura za urais,” aliambia Taifa Jumapili.

Dkt Mutua ametangaza wazi kwamba safari yake ya kwenda Ikulu imeshaanza, kauli ambayo imeibua uhasama kati yake na makamu wa rais wa zamani na kigogo wa siasa za Ukambani, Bw Kalonzo Musyoka, ambaye pia anamezea mate kiti cha urais.

“Kwa neema ya Mungu nitakuwa rais wa tano wa Kenya,” akasema Dkt Mutua.

Gavana wa Muranga Mwangi Wa Iria, 47, ni miongoni mwa vigogo wa Mt Kenya walio na matumaini ya kunyakua uongozi wa taifa.