Magavana 3 wa Pwani mbioni kujijengea jina

Magavana 3 wa Pwani mbioni kujijengea jina

Na WAANDISHI WETU

MAGAVANA watatu wa kaunti za Pwani ambao wanatumikia hatamu yao ya mwisho mamlakani, wako mbioni kujijengea sifa kabla wang’atuke mwaka 2022.

Magavana hao ambao ni Salim Mvurya (Kwale), Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi) wameweka kipaumbele miradi ya elimu na maendeleo yanayoinua jamii kimaisha.

Katika Kaunti ya Kwale, Bw Mvurya anajitahidi kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha matunda kwa gharama ya Sh600 milioni katika eneo la Shimba Hills.

Mkuu wa wafanyakazi katika kaunti hiyo, Bw Rodgers Chimega alisema ujenzi wa kiwanda hicho ulianza mwaka wa 2019 na awamu ya pili ikaanza mwaka uliopita.

Mradi mwingine ambao Bw Mvurya ameupa kipaumbele ni ujenzi wa taasisi ya mafunzo ya ualimu. Mradi huo unatarajiwa kugharimu Sh300 milioni na ukikamilishwa itakuwa mara ya kwanza kaunti hiyo kuwa na taasisi ya mafunzo ya ualimu ambayo itakuwa ya pili kwa ukubwa eneo la Pwani.

“Huo mradi uko karibu kukamilika na tayari tumeanza kutafuta wahadhiri kabla taasisi ifunguliwe rasmi,” akasema Bw Chimega.

Alisema serikali ya kaunti hiyo inatarajia kukamilisha soko la mazao ya shambani la Kombani katika Kaunti Ndogo ya Matuga ambayo bajeti yake ilikuwa ya kugharimu Sh120 milioni.

Soko hilo lililo karibu na barabara ya Likoni-Lunga Lunga-Dar es Salaam ambalo ujenzi wake ulianza mwaka wa 2019, halijakamilika lakini serikali ya kaunti hiyo inasema linatarajiwa kukamilika kufikia mwezi ujao.

Katika Kaunti ya Mombasa, utawala wa Bw Joho umeupa kipaumbele ujenzi wa nyumba za bei nafuu, miundomsingi na afya anapokaribia kukamilisha hatamu yake ya mwisho ya uongozi.

Miradi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu inaendelezwa katika mitaa ya Buxton, Likoni, na Changamwe kwa ushirikiano na serikali kuu.

“Mradi wa Buxton tayari umeanza lakini ile ya Likoni na Changamwe bado. Waekezaji wamejitolea na haitachukua muda mrefu kabla miradi yote ipige hatua,” akasema Kaimu Katibu wa Kaunti, Bw Joab Tumbo.

Bw Joho pia anaendelea kuwekeza kiasi kikubwa cha bajeti za serikali yake kwa utoaji wa huduma bora za afya katika hospitali za umma, huku lengo likiwa ni kuhakikisha hospitali zote za kaunti ndogo sita zinahudumu bila matatizo.

Vile vile, kaunti hiyo inatarajia kushirikiana na serikali kuu kwa ujenzi wa maeneo maalumu ya kiviwanda Miritini na Dongo Kundu. Serikali kuu ilitenga Sh8.5 bilioni kwa ujenzi wa eneo la Dongo Kundu.

Kwa upande wake, Bw Kingi anajitahidi kukamilisha ujenzi wa jengo jipya la matibabu katika Hospitali ya Kaunti ya Kilifi, na kukamilisha kulipa madeni ya kaunti kabla aondoke mamlakani.

Haya ni kwa mujibu wa bajeti ya 2020/2021 ya kaunti hiyo ambapo bunge la kaunti lilikubali kuwa kuna haja ya kukamilisha kulipa madeni yote kabla Uchaguzi Mkuu ujao.

Ujenzi wa jengo jipya la hospitali ulikuwa umeanzishwa mwaka wa 2018 ambapo awamu ya kwanza ilitengewa Sh300 milioni huku Benki ya Dunia ikifadhili mradi huo kwa Sh150 milioni.

Magavana wengine wa kaunti ambao wanatumikia awamu yao ya kwanza, pia wanajitahidi ili kuwaridhisha wapigakura kabla uchaguzi wa mwaka ujao ufike.

Magavana hao ni Dhadho Godhana wa Tana River, Granton Samboja wa Taita Taveta na Fahim Twaha wa Lamu.

Ripoti za Siago Cece, Kalume Kazungu, Lucy Makanyika, Stephen Odour na Maureen Ongala

You can share this post!

Thierry Neuville amwaga Sh257,000 milioni kusaidia ndovu na...

Chai: Bomet yapata soko Iran