Habari MsetoSiasa

Magavana kupinga uamuzi wa kufurushwa ofisini

December 16th, 2019 1 min read

Na AGGREY OMBOKI

BARAZA la Magavana linawazia kwenda mahakamani kupinga agizo ambalo huhitaji magavana kutoingia afisini wanaposhtakiwa kwa madai ya ufisadi.

Agizo hilo lilianza kutolewa wakati Jaji Mumbi Ngugi alipomfungia nje Gavana wa Samburu, Moses Lenolkulal.

Akizungumza Nairobi jana, Mwenyekiti wa baraza hilo aliye pia Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya alisema agizo hilo limeathiri sana shughuli za kaunti tatu ambazo magavana wao wamezuiliwa kuingia afisini.

Wanajumuisha Bw Lenolkulal, Ferdinand Waititu wa Nairobi na Mike Sonko wa Nairobi.

Bw Oparanya alisema watatafuta ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu kando na kuelekea katika Mahakama ya Juu.

Kulingana naye, hali inayoshuhudiwa Nairobi kufuatia masaibu ya Bw Sonko ni ambayo haijawahi kuonekana nchini.

“Tutahitaji ufafanuzi wa uamuzi uliotolewa na Jaji Mumbi Ngugi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu au hata katika Mahakama ya Juu,” akasema Bw Oparanya.

Kaunti ya Nairobi haijakuwa na Naibu Gavana tangu aliyekuwa naibu, Polycarp Igathe alipojiuzulu ghafla mnamo Januari mwaka uliopita.

Miongoni mwa watu ambao Sonko alikuwa amependekeza wawe naibu wake ni mwanasiasa mtatanishi Miguna Miguna ambaye alifurushwa nchini.

Bw Miguna jana alitangaza kwenye mitandao ya kijamii kwamba amepanga kurudi nchini Januari mwaka ujao.

Bw Sonko bado anatarajiwa kushtakiwa kwa madai ya kulumbana na polisi alipokuwa akikamatwa.

Kesi hiyo imepangwa kufanyika kesho katika Mahakama ya Voi.