Habari

Magavana kusimamisha huduma za kaunti zote 47

August 30th, 2019 1 min read

Na COLLINS OMULO

MAGAVANA wametishia kusitisha shughuli katika serikali za kaunti kote nchini kuanzia Septemba ikiwa mzozo kuhusu ugawaji wa mapato hautakuwa umesuluhishwa.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), Wycliffe Oparanya alisema Alhamisi ikiwa mazungumzo yanayolenga kutatua mvutano kuhusu kiasi cha fedha zinazopasa kutengewa serikali za kaunti hayatazaa matunda, kaunti zote zitasitisha huduma kuanzia Septemba 16.

“Jinsi mnavyofahamu, suala hilo haliko mikononi mwetu sisi kama magavana. Linajadiliwa na bunge la Kitaifa na lile la Seneti. Tunatarajia kwamba watasuluhisha suala hilo haraka ili kukomesha matatizo yanayoshuhudiwa katika kaunti.

“Baada ya tarehe hii, ikiwa mvutano huo hautatatuliwa basi tumeamua kwamba serikali za kaunti hazitakuwa na lingine mbali kusitisha shughuli,” akaeleza Bw Oparanya.

Mwenyekiti huyo, ambaye pia ni Gavana wa Kakamega, alisema hayo katika kikao na wanahabari baada ya kuongoza mkutano wa uongozi wa CoG katika makao makuu ya baraza hilo jijini Nairobi.

Mvutano huo umesababisha changamoto za kifedha katika kaunti nchini na kuchangia migomo ya wanafanyakazi wanaolalamikia kutolipwa mishahara ya mwezi wa Julai.

Kujizatiti

Bw Oparanya alisema kaunti chache zimekuwa zikijizatiti kulipa mishahara ya wafanyakazi wao, lakini hali imekuwa mbaya zaidi kiasi kwamba hazitaweza kulipa mishahara mwishoni mwa mwezi huu.

“Mvutano huu kati ya wabunge na maseneta umechangia baadhi ya kaunti kukosa kulipa mishahara ya wafanyakazi wao kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita. Imetubidi kuwapa tahadhari wafanyakazi wawe tayari kwa hali ngumu zaidi mwezi ujao,” akasema.

Wabunge wanataka serikali za kaunti zipewe Sh316 bilioni katika mwaka huu wa kifedha wa 2019/2020 huku maseneta wakipendekeza mgao wa Sh335 bilioni.

Mnamo Juni pande hizo mbili zilikosa kuelewana hata baada ya maspika wa mabunge hayo mawili kuunda kamati ya upatanishi.