Habari Mseto

Magavana Pwani wakaa ngumu kuhusu muguka, wasema hawakutani ng’o na Linturi

June 6th, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

SERIKALI ya kitaifa sasa imejipata katika njiapanda, baada ya magavana wa Pwani kukataa kuhudhuria mkutano wa kujadili suala la muguka.

Magavana Abdulswamad Nassir (Mombasa), Gideon Mung’aro (Kilifi), Fatuma Achani (Kwale), Dhado Godhana (Tana River), Issa Timmamy (Lamu) na Andrew Mwadime (Taita Taveta) walitoa uamuzi huo Jumatatu.

Vilevile maseneta, wabunge na viongozi wengine wa Pwani wamesema hawatahudhuria mkutano huo ambao uliagizwa na Rais William Ruto kusaka mwafaka baada ya magavana watatu wa eneo hilo, Bw Nassir, Bw Mung’aro na Bw Mwadime kupiga marufuku biashara na utafunaji wa muguka huku Bi Achani akiunga mkono ada za juu za bidhaa hiyo Kwale.

Wiki iliyopita, Rais Ruto alikutana na viongozi wa Embu akiongozwa na Gavana Cecily Mbarire na kushtumu hatua ya magavana wa Pwani kupiga marufuku zao hilo linalozolea taifa faida. Vile vile aliahidi Sh500 milioni kukuza zao hilo.

Rais Ruto akamwagiza Waziri wa Kilimo Bw Mithika Linturi kuandaa kikao maalum na magavana wa Pwani ili kuafikiana kuhusu marufuku dhidi ya muguka.

“Tulipata mwaliko wa kuhudhuria mkutano nawe (Waziri), lakini tungependa kukufahamisha kuwa hatuwezi kukutana na wewe kwa sababu ya msimamo wako kuhusu muguka. Umenukuliwa ukisema muguka ni halali na hauwezi kupigwa marufuku na magavana,” Magavana wa Pwani kupitia Jumuiya ya Kaunti za Pwani walisema.

Kwenye barua waliyomwandikia Bw Linturi, magavana hao wakiongozwa na mwenyekiti wa JKP, walisema waziri huyo hawezi kusimamia mkutano wa kujadili mmea ambao ameutetea.

“Usemi wako kuhusu muguka unaonyesha unatetea zao hili. Umepuuza msimamo wetu ambao unatetea afya ya wapwani. Ndio maana hatutahudhuria mkutano wako sababu utakuwa na upendeleo,” waliongeza.

Walisema sababu Rais alikutana na viongozi wa maeneo ambayo linakuzwa zao hilo, nao pia wana haki ya kukutana naye.

“Mnamo Mei 29, 2024, Rais alikutana na viongozi wa maneo yanayokuza muguka, pia sisi tunataka mkutano naye tumuelezee changamoto zetu kuhusu muguka,” wakasema.

Walisema mkutano huo pia ujumuishe wataalamu, mashirika ya kijamii, shirika la kitaifa la kupambana na dawa za kulevya, vyombo vya usalama na Wizara ya Afya sababu swala la muguka si la kilimo pekee bali hata afya, uchumi na usalama.

Bw Mung’aro alisema viongozi wa Pwani hawatakubali kutishiwa sababu ya msimamo wao wa kupiga marufuku muguka.

Mnamo Jumatatu, wanasiasa wa Pwani walimshtumu Rais Ruto kwa kuendeleza ubaguzi baada ya kukutana na wanasiasa wa Embu kutokana na hatua ya Magavana wa Pwani kupiga marufuku muguka.

Wanasiasa hao kutoka mirengo tofauti ikiwemo chama tawala cha UDA, PAA, upinzani ODM, walisema mkutano wa Rais na viongozi wa Embu akiongozwa na Gavana Cecily Mbarire na hata kufadhili ukuzaji wa muguka ni kejeli kwa viongozi wa Pwani.

Wafanyabiashara walienda mahakama kushtaki magavana wa Pwani waliopiga marufuku muguka.

Mahakama Kuu huko Embu iliondoa marufuku hiyo ikisubiri kusikiza kesi hiyo.

Kulingana na utafiti mbali mbali, matumizi ya muguka huwa na athari mbali mbali za kiafya ikiwemo kurukwa na akili.

Viongozi wa Pwani walisema ni kejeli kwa Rais kuamuru Waziri Linturi kukutana nao ilhali alikutana ana kwa ana na viongozi wa Embu.

“Rais ni rafiki yangu lakini ametubagua kwenye maamuzi yake kuhusu muguka,” alisema Mbunge wa Kilifi Kaskazini Bw Owen Baya kwenye mkutano wa Muungano wa Wabunge wa Pwani, katika hoteli ya Pride Inn Paradise.